DC Mapunda ataka manispaa Dar kutumia Jeshi la Akiba


Na MWANDISHI WETU

MKUU wa Wilaya  ya  Temeke, Sixtus Mapunda, amezielekeza halmashauri za manispaa zote mkoani Dar es Salaam, kuhakikisha zinawatumia kikamilifu  wahitimu wa mafunzo ya awali ya Jeshi la Akiba katika utekelezaji wa operesheni mbalimbali.


Ametoa maelekezo hayo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, katika hafla ya ufungaji wa Mafunzo ya Awali ya Jeshi la Akiba  Kundi  la 63/2025 yaliyofanyika katika viwanja vya Kambi ya Jeshi la Wanamnchi Tanzania ya  Twalipo, wilayani Temeke.


“Manispaa zote katika shughuli zao na operesheni zao ziwatumie  vijana hawa. Wakurugenzi muwatumie wahitimu hawa  haraka kabla hawajarudi mtaani,”amebainisha  Mapunda.


 Amesema  vijana hao wakiachwa  mtaani kwa kipindi kirefu  bila kutumika  watasahau kwa haraka kiapo chao.


“Tuna operesheniu za kukusanya mapato. Tuna maandalizi ya uchaguzi mkuu na kusimamia taratibu mbalimbali katika manispaa zetu. Hawa vijana  wako tayari kutumika,”ameeleza Mapunda.


Aidha, ametoa  wito kwa wahitimu hao  kushiriki kikamilifu katika uchaguzi mkuu  unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29 mwaka huu.


“ Oktoba 29 ni siku ya uchaguzi mkuu. Tujitokeze kwa wingi kupiga kura. Ninawakabidhi jukumu la kwenda  kuhamasisha vijana wenzenu kujitokeza kupiga kura,”amesema.


Mapunda amewataka wahitimu hao kuishi kwa kiapo na kujiepusha kutumia mafunzo waliyopata  katika vitendo viovu.


Awali Mshauri wa Jeshi la Akiba Mkoa wa Dar es Salaam, Kanali Emmanuel Kasyupa, alisema mafunzo hayo  yalijumuisha vijana kutoka wilaya tano za mkoa huo ambazo ni Ilala, Temeke, Kinondoni, Kigamboni na Ubungo.


“Mafunzo  yalianza Aprili nne mwaka huu yakiwa na wanafunzi   414. Wanafunzi 66 walishindwa kuendelea  kutokana na sababu  mbalimbali zikiwemo za utoro, matatizo ya afya na  utovu wa nidhamu,”alieleza Kanali Kasyupa.


Amesema  jumla ya wahitimu wote ni  348, wanaume  263  na wasicha 85 ambapo mafunzo hayo yalifanyika kwa wiki 18.


Kanali Kasyupa alibainisha, wakufunzi walitoka Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), Jeshi la Polisi, Uhamiaji, Usalama wa Taifa na  Jeshi la Zimamoto na Uokoaji.


“Kiapo kimesikika. Mmeahidi kuwa watiifu na waaminifu  kwa Amirijeshi Mkuu  wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na mtakuwa watiifu kwa raia. Usiende kukiweka  kiapo hiki katika begi,  Ikiwezekana ubandike sebuleni ili mgeni akija atambue unawajibu gani kwa taifa,”ameebainisha.


Amesisitiza  wahitimu hao  kulinda  uhuru na uchumi  wa nchi kama walivyo apa.

“Askari hawa  wamefikia kiwango kinachokubarika  katika jeshi la akiba na wapo tayari kutumikia  taifa katika kutekeleza majukumu mbalimbali,”ameeleza Kanali Kasyupa.


Katika mafunzo yao wahitimu hao walipata masomo mbalimbali kwa nadharia  na vitendo, ikiwa ni pamoja na kwata, ukakamavu, mbinu za kivita, ujanja wa porini, usomaji ramani, huduma ya kwanza, zimamoto, uhamiaji, usalama wa taifa, Kuzuia na kupambana na rushwa, silaha ndogondogo, utimamu wa mwilki, uraia, kazi za polisi, uhamdisi wa medani,Sheria za Jeshi la Akiba na vita vya  msituni.


Katika risala yao  wahitimu hao waliiomba serikali kuongeza bajeti ya mafunzo ya jeshi la akiba na kuwapa kipaumbele  kujiunga na JKT  na  taasisi zingine za aserikali. 



DC Mapunda ataka manispaa Dar kutumia Jeshi la Akiba DC Mapunda ataka manispaa Dar  kutumia  Jeshi la Akiba Reviewed by Gude Media on 8:49:00 PM Rating: 5

No comments

Note: Only a member of this blog may post a comment.