Diwani Klerruu: Rais Dk. Samia ameandika historia utekelezaji miradi ya miundombinu Kata ya Mabibo


Na MWANDISHI WETU

Diwani wa Kata ya Mabibo, wilayani Ubungo, mkoani Dar es Salaam, Joseph Klerruu, ameishukuru na kuipongeza serikali chini ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan na wasaidizi wake kwa  utekelezaji miradi ya maendeleo yenye thamani ya Sh. bilioni 15.2 katika  kata hiyo.

Klerruu amesema  utekelezaji huo wa miradi umevunja rekodi katika  kata hiyo tangu Tanzania ilipopata uhuru mwaka 1961, ambapo Sh.  12,315,000,000 kimeelekezwa katika ujenzi, uboreshaji na ukarabati wa miundombinu.

Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa mwaka wa  fedha 2020-2025 katika Baraza Maalumu la  Umoja wa Vijana wa Chamama Cha Mapinduzi (UVCCM) Kata ya Mabibo, Dar es Salaam, amesema fedha hizo zimetumika katika utekelezaji wa miradi kwa mwaka huo wa fedha, ikihusisha sekta zote zikiwemo za miundombinu, afya, elimu, maendeleo ya jamii, biashara, masoko, ulinzi na usalama, utawala, michezo na utamaduni.

Klerruu amesema miongoni mwa miradi iliyotekelezwa ni ujenzi wa barabara ya lami  ya NIT- Madoto Mburahati yenye urefu wa Kilometa 1.8  na taa zake  iliyogharimu sh.  8,000,000,000.

“Aidha tumefanya ukarabati kwa Barabara Mabibo Mwisho- Maungio ya Barabara ya Morogoro na taa zake yenye urefu wa kilometa 1.2 kwa gharama ya sh. 4,000,000,000,”amesema

Amesema  kamati ya maendeleo ya kata iliyo chini ya usimamizi wake ilifanikisha ukarabati wa Barabara ya Ushese Kilometa 0.770, Mtaa wa Jitegemee kwa gharama ya sh. 5,000,000 ambapo ukarabati kama huo umefanyika,  katika Barabara ya VINA, Mtaa wa Azimio kwa kiwango hicho hicho cha fedha.
 
“Pia  tumefanya ukarabati wa Barabara ya Msikitini- kwa Mzee Mndenge, ukarabati umefanyika mara tatu lakini ukihusisha kipande cha Mabibo Sekondari, Zahanati ya Mabibo, Kanisa la Kiinjili la Kilutheri  Tanzania (KKKT) na Mwembeni Mtaa wa Mabibo Farasi. Kiasi cha shilingi milioni sitini  kimetumika,”ameeleza.
 
Klerruu amesema ukarabati wa Kalvati eneo la AMI kwa gharama ya  sh.20,000,000, ujenzi wa Kalvati eneo la Kanisa la KKKT MabiboUpogoroni kwa  gharama ya sh.18,000,000 na ujenzi wa Kalvati  katika eneo maarufu kwa Mzee Likonga Mabibo Farasi kwa gharama ya sh.20,000,000.

“Kubwa zaidi ni ujenzi wa kivuko cha waenda kwa miguu maarufu Kivuko cha Gonzaga kwa gharama ya  ya shilingi milioni miamoja na tatu. Pia tumefanikisha ukarabati wa Barabara ya Makutano  kwenda kwa Binti Kayenga, Luhanga yenye urefu wa kilometa 1.3 kwa gharama ya shilingi milioni miamoja alizotoa Rais Dk. Samia kupitia mfuko  wa Jimbo,”amesema Klerruu.

Pia, Klerruu amesema chini ya Rais Dk. Samia, ujenzi wa Barabara ya Zege yenye urefu wa kilometa 1.87 kutoka TIP TOP, Makutano, Binti Kuyenga  inatarajiwa kujengwa kwa  gharama ya Sh. 2,500,000,000.

“Ujenzi utaanza muda wowote kuanzia sasa chini ya Mradi wa  Uboreshaji wa  Miundombinu ya Jiji la Dar es Salaam (DMDP) Tuynamshukuru Rais Dk. Samia,”amesema.
Diwani  huyo  ambaye pia ni Mtaalamu wa Masuala ya Ardhi na Majenzi alieleza  kufanyiwa kwa uthamini wa mali za wananchi kupisha ujenzi wa Barabara ya Mwananchi- AMI-Zahanati-Miembeni Mabibo Farasi.

“Kukamilika kwa ujenzi wa barabara hii kutaondoa msongamano wa magari kwenda Buguruni kwa wale wenye nia ya kuelekea Magomeni, Kinondoni, Oysterbay na Masaki,”ameeleza Diwani Klerruu.
Alisema  kiasi cha sh.12,315,000,000 kimetumika katika sekta ya miundombinu na kwa ujumla kwa kipindi cha Mwaka 2020-2025.

Klerruu amewaomba wananchi wa Kata ya Mabibo, kuendelea kumuamini yeye, Rais Daktari Samia na CCM katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwezi Oktoba 2025 kwani kazi iliyofanyika ni kubwa na Mabibo inapiga hatua kubwa kwa Maendeleo.

Uongozi wa Baraza la UVCCM Kata ya Mabibo umepokea taarifa hiyo na kumpongeza diwani huyo kwa Utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM na kuahidi ushindi mkubwa wa katika Uchaguzi Mkuu wa Mwaka huu wa Rais, Mbunge na Diwani.

Diwani Klerruu: Rais Dk. Samia ameandika historia utekelezaji miradi ya miundombinu Kata ya Mabibo Diwani Klerruu: Rais Dk. Samia ameandika  historia utekelezaji miradi ya miundombinu Kata ya Mabibo Reviewed by Gude Media on 3:54:00 AM Rating: 5

No comments

Note: Only a member of this blog may post a comment.