Arusha, 22 Novemba 2026
Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, anaondoka nchini leo, tarehe 22 Novemba, 2026, kuelekea Addis Ababa, Ethiopia kwa Ziara ya Kikazi ya siku mbili.
Akiwa Kinara wa Umoja wa Afrika wa Afya ya Uzazi, Mama na Mtoto, Rais Dkt. Samia atashiriki Mkutano wa Tano wa Kimataifa wa Afya ya Umma Barani Afrika (CPHIA 2026), na kuzindua Mpango Elekezi wa Kuboresha Afya ya Mama na Mtoto Barani Afrika, tarehe 23 Novemba, 2026.
Mpango huo unalenga kuongoza nchi wanachama wa Umoja wa Afrika kufikia malengo yajulikanayo kama Sifuri Tatu (Three Zeros), ambayo ni:
1. Kuhakikisha kila mjamzito anajifungulia katika kituo cha kutolea huduma za afya akisaidiwa na mtaalamu;
2. Kukomesha vifo vitokanavyo na uzazi na vya watoto wachanga, vinavyoweza kuzuilika; na
3. Kuhakikisha kila mtoto anapata chanjo.
Mpango Elekezi wa Kuboresha Afya ya Mama na Mtoto Barani Afrika utatekelezwa kuanzia mwaka 2026 hadi 2030, ukilenga kuongeza uwekezaji wa nchi wanachama na wadau wa maendeleo katika kupanua upatikanaji wa huduma bora za afya kwa wanawake, watoto na vijana barani Afrika.
Taarifa hiyo imetolewa na Bakari S. Machumu, Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu.
