Na MWANDISHI WETU, Kigamboni
DIWANI wa Kata ya Kigamboni, Dotto Msawa, amesema zaidi ya wananchi 2,000 wenye matatizo ya macho wamepatiwa matibabu ya bure na kugaiwa miwani kupitia kambi maalumu ya matibabu katika Kituo cha Afya Kigamboni.
Akizungumza katika ufungaji wa kambi hiyo, Dotto amesema huduma hizo zimekuwa msaada mkubwa kwa wananchi wa kipato cha chini ambao wasingeweza kumudu gharama za matibabu ya macho zinazoweza kufikia kati ya Sh. 400,000 na 500,000 kwa mtu mmoja.
Amesema huduma hizo zimepatikana kutokana na msaada wa Serikali ya Kuwait kupitia taasisi ya Majay Foundation, kwa lengo la kuwasaidia wananchi wa Kigamboni na maeneo jirani kupata huduma za afya bila gharama.
"Tunamshukuru Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa juhudi zake za kuimarisha ushirikiano na mataifa mbalimbali katika kutafuta misaada yenye manufaa kwa Watanzania, akieleza kuwa hatua hiyo imekuwa na mchango mkubwa katika kuwafikia wananchi wenye uhitaji, wakiwemo wananchi wa kata hiyo", amesema.
Dotto amesema kambi hiyo haikuhudumia wakazi wa kata hiyo pekee, bali iliwafikia wananchi kutoka maeneo mbalimbali ya Wilaya ya Kigamboni, yakiwemo Pembanazi, Kisarawetu na Vijibweni, baada ya matangazo ya huduma hizo kusambazwa katika maeneo mbalimbali ya wilaya.
Amesema juhudi hizo ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) na kuunga mkono kazi zinazofanywa na Rais Dk. Samia, wabunge na madiwani katika kuwaletea wananchi maendeleo.
Kwa upande wa Daktari Mfawidhi wa kituo hicho, Peter Nyang’anyi amesema kambi hiyo imefanikiwa kuwafikia zaidi ya wananchi 2,000, ambao walipata huduma mbalimbali zikiwemo vipimo vya macho, miwani, ushauri na matibabu stahiki na huduma za upasuaji kwa wagonjwa waliokuwa na uhitaji huo.
Amesema baadhi ya matatizo ya macho yanatokana na changamoto za kuzaliwa nazo, ambazo zinaweza kuhusishwa na mambo mbalimbali yanayotokea wakati wa ujauzito.
Aidha Dk. Nyang’anyi amewataka wananchi kuendelea kufuatilia elimu ya afya, kuzingatia lishe bora, kufanya uchunguzi wa afya mara kwa mara na kuwahi hospitalini wanapobaini changamoto za kuona.
Naye Daktari wa Macho na Mratibu wa Huduma za Macho katika Manispaa ya Kigamboni, Josephine Ngonyani, amesema huduma za macho zimekuwa miongoni mwa huduma zinazokabiliwa na changamoto mbalimbali, ikiwemo gharama kubwa za matibabu, wingi wa magonjwa ya macho na uelewa mdogo wa wananchi kuhusu matatizo ya macho na mahali sahihi pa kupata matibabu.
Dk. Josephine amesema kambi hiyo imetoa elimu maalumu kuhusu ugonjwa wa presha ya macho, ambao kwa muda mrefu umekuwa ukizungukwa na dhana potofu katika jamii, huku baadhi ya watu wakiuhusisha na imani za kishirikina badala ya kuelewa kuwa ni tatizo la kiafya linalohitaji uchunguzi na matibabu ya kitaalamu.
Mmoja wa wananchi waliopata huduma ya macho katika kambi hiyo, Catherine Mwenda, amesema shida yake ilikuwa jicho la kushoto lilikuwa linauma, lakini sasa linaendelea vizuri baada ya kupata matibabu kutoka kwa madaktari.
"Nilipopata taarifa kuna huduma inatolewa hapa ya upimaji wa macho na matibabu bure na mimi nikafuatilia, hatimaye nikapata huduma nzuri sana, kwanza wanatujali wazee na tumehudumiwa vizuri", amesema.
