Chuo cha Bandari Kuzalisha Wataalamu Wenye Ufanisi wa Kimataifa


Na MWANDISHI WETU

MKUU wa Chuo Cha Bandari, Dk. Lufunyo Hussein, amesema wanafanya jitihada kubwa za kuzalisha wataalamu wenye ufanisi mkubwa unaoendana na uhitaji wa soko la sasa na kukidhi viwango vya kimataifa.

Pia, amemshukuru Rais Dk.Samia Suluhu Hassan kwa kutenga fedha za kutosha kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) za kujenga miundombinu mbalimbali ya kufundishia na kufanyia tafiti chuoni hapo ikiwemo mahabara ya kisasa na majengo ya kujifunzia na kufanya tafiti,kwa lengo la kupata wataalamu bobezi.

Dk. Hussein aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam, alipozungumza na waandishi wa habari kuhusu maandalizi ya mahafali ya 25 yatakayo fanyika kesho Novemba 25, mwaka huu, Chang'ombe Dar es Salaam.

"Chuo Cha Bandari kimepata Ithibati ya ubora wa Kimataifa, hivyo hata mitaala yetu lazima iendane na ubora huo kupata wataalamu wanaokidhi uhitaji wa ndani na wa kimataifa," amesema.

Amesema wamedhamiria kuzalisha nguvu kazi ambayo ni shindani kulingana na soko la kimataifa kwani bila kufanya hivyo zinaweza kujitokeza fursa za ajira zisiwe na tija kwa vijana wa hapa nchini.

Akielezea kuhusu mahafali yatakayofanyika kesho wilayani Temeke, amesema maandalizi yako vizuri na wanatarajiwa mgeni rasmi atakuwa Mwenyekiti wa Bodi, Balozi Ernest Mangu.

Akitaja idadi ya wahitimu wanaotarajiwa kuhitimu katika mahafari hayo ya 25, amesema wanaotarajiwa kuwa 819, wakiume 382 na wakike ni 437 wakihitimu Astashahada, Stashahada.

Akifafanua kuhusu ujenzi na uboreshaji wa majengo ya kisasa chuoni hapo, alisema unaendelea kutekelezwa vyema kwa lengo la kuhakikisha wanaongeza wigo wa wanafunzi wa kozi za muda mrefu na zile za muda mfupi.