THBUB, DIHR Kuimarisha Ushirikiano katika Ulinzi wa Haki za Binadamu

 

WENYEKITI wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), Wakili Dunford Mpelumbe, amesema ushirikiano kati ya tume hiyo na Taasisi ya Haki za Binadamu ya Denmark (DIHR) umechangia kwa kiasi kikubwa kuimarisha juhudi za kukuza na kulinda haki za binadamu nchini, hususan katika masuala ya biashara na haki za binadamu pamoja na usimamizi endelevu wa rasilimali za bahari.

Wakili Mpelumbe ameyasema hayo alipokutana na ujumbe wa DIHR uliohusisha Mshirika wa Biashara na Mdhibiti wa Miradi pamoja, Katrina Palad na Mshauri wa Haki za Binadamu, Biashara na Teknolojia, Bernard Ochieng, katika Ofisi za Tawi la THBUB jijini Dar es Salaam.

Wakili Mpelumbe amesema, ushirikiano huo ulioanza mwaka 2017 umewezesha tume kutekeleza afua mbalimbali, zikiwemo kufanya tathmini ya hali ya biashara na haki za binadamu nchini, kuandaa Mpangokazi wa Taifa wa Biashara na Haki za Binadamu, kujenga uwezo wa watumishi na kuimarisha mifumo ya ufuatiliaji pamoja na upatikanaji wa haki kwa waathirika wa ukiukwaji wa haki zinazohusiana na shughuli za biashara.

“Tunathamini sana ushirikiano wa muda mrefu na wa kimkakati kati ya taasisi zetu mbili, ambao umechangia kwa kiasi kikubwa katika kukuza na kulinda haki za binadamu nchini ,” ameeleza Wakili Mpelumbe.

Aidha, amebainisha katika eneo la usimamizi wa rasilimali za bahari, THBUB imefanya uchambuzi kuhusu haki za wavuvi wadogo na upatikanaji wa rasilimali za baharini kwa kuzingatia misingi ya haki za binadamu.

"Juhudi hizo zimechangia kuongeza uelewa wa jamii za pwani kuhusu haki zao, ushiriki katika maamuzi na mifumo ya kuwasilisha malalamiko na kupata suluhu," alieleza.

Kwa upande wake, Ochieng, alimpongeza Mwenyekiti wa THBUB pamoja na Makamu Mwenyekiti kwa uteuzi walioupata, akiwatakia mafanikio katika majukumu yao na kusishukuru tume kwa ushirikiano mzuri uliowezesha DIHR kutekeleza shughuli zake kwa mafanikio na kuahidi kuendeleza ushirikiano huo wenye tija.