FCC Yaendelea Kuimarisha Utoaji wa Huduma kwa Umma Kupitia Mfumo wa Kidijitali wa FCC Automation


Na MWANDISHI WETU

Tume ya Ushindani (FCC) inaendelea na utekelezaji wa mradi wa uandaaji wa mfumo wa kisasa wa kidijitali wa utendaji kazi wa Taasisi (FCC Automation), unaolenga kuboresha ufanisi wa kiutendaji, kurahisisha upatikanaji wa huduma na kuongeza tija katika utoaji wa huduma kwa Umma na wadau wake.

Hayo yamebainishwa na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Ushindani (FCC), Khadija Ngasongwa, alipofanya ziara ya kutembelea na kukagua maendeleo ya mradi huo , katika kikao kazi cha majaribio na mapitio ya mfumo (FIMS UAT Workshop) kinachofanyika katika Hoteli ya Nashera, mkoani Morogoro.

Katika ziara hiyo, Ngasongwa alipata fursa ya kupatiwa maelezo na wataalam kuhusu hatua mbalimbali zilizofikiwa katika uandaaji wa mfumo huo, hususan maendeleo ya kiufundi, utendaji na ufanisi wa mfumo, kupitia ushirikiano wa watumishi wa FCC kutoka Kurugenzi na Idara mbalimbali za Taasisi, pamoja na wataalam na wakandarasi wanaosimamia utekelezaji wa mradi kutoka ICTPACK, ICT FCC na TMA.

Mradi huo ulioanza kuandaliwa takribani miaka miwili iliyopita, unatarajiwa kukamilika mwezi Juni 2027. Mfumo huo unaotumia teknolojia ya mtandao (Web-based System) utawezesha FCC kuboresha mifumo yake ya ndani ya kiutendaji sambamba na kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa Umma na wadau mbalimbali wa Taasisi.

Kupitia mfumo huo, wadau na wananchi wataweza kupata huduma za FCC kwa njia ya kielektroniki, ikiwemo usajili, kuwasilisha maombi ya huduma mbalimbali na kupata huduma zinazohusiana na shughuli za makampuni, kama vile uunganishaji wa miamala ya makampuni, ongezeko la mitaji na huduma nyingine zilizo chini ya mamlaka ya Tume. Hali hiyo itapunguza utegemezi wa taratibu za kawaida za ana kwa ana na kuwawezesha wadau kupata huduma kwa urahisi zaidi.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Ngasongwa alieleza kuwa kukamilika kwa mfumo huo kutaiwezesha FCC kuwa na nyenzo madhubuti za kiteknolojia zitakazoongeza ufanisi wa kazi, kuimarisha usimamizi wa shughuli za Taasisi na kuboresha utoaji wa huduma kwa Umma.