MENEJA wa Huduma kwa wateja wa Shirika la Mawasiliano, TTCL, Diwani Mwamengo amesema wataendelea kuongeza kasi ya kuimarisha huduma zake za mawasiliano, intaneti ya Faiba, Teknolojia, habari na Mawasiliano (TEHAMA), kwa lengo la kuwapatia wananchi huduma bora na kutatua changamoto zako kwa wakati.
Amesema hayo, jana, Dar es Salaam, kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa TTCL, Moremi Marwa, katika kilele cha maadhimisho ya wiki ya huduma kwa mteja, kilichofanyika Makao Makuu ya TTCL, huku akitaja Kauli mbiu ya wiki hiyo ni “ Kwenda hatua ya ziada katika kumhudumia mteja”
“Mteja anaweza kuvutiwa na huduma zetu za mawasiliano na teknolojia, lakini ataendelea kuwa na sisi kwasababu ya ubora wa huduma tunazompatia, hivyo kila mfanyakazi ana nafasi muhimu katika kuboresha huduma na kuongeza ushindani wa kuhudumia wateja.
Amesisitiza kila mteja anapate huduma bora zaidi kwa kusikilizwa, kuthaminiwa na kuhakikisha changamoto zake zinapatiwa ufumbuzi kwa haraka.
Amewataka wafanyakazi wa shirika hilo kuimarisha utoaji hduma kwa wateja, kupokea maoni, ushauri, kupokea malalamiko kama taarifaa muhimu ya kusaidia kubaini maeneo yanayohitaji maboresho. Ni wajibu wao kuhakikisha kila mteja anapatiwa ufumbuzi wa changamoto ya malalamiko yake badala ya kuonekana kama kero.
Kwa upande wake, Mdau wa huduma za TTCL, Mnandwa Maulid Mnandwa, ambaye ni Rais wa Serikali ya wanafunzi wa Chuo Cha Biashara (CBE), jijini Dar es Salaam, alipongeza shirika hilo kwa maadhimisho ya wiki hiyo ya huduma kwa wateja, kwa namna walivyo wahudumia watu mbalimbali ikiwemo kufikisha huduma za intaneti chuoni hapo, wakiahidi ushirikiano wakati wote.

.jpeg)
