Na MWANDISHI WETU
WANANCHI, wadau, taasisi, mashirika,kampuni na watu binafsi wameombwa kujitokeza kusaidia kufanikisha harambee inayo lenga kukusanya Sh. milioni 105 kusaidia ununuzi wa vifaa muhimu vya afya wilayani Kigamboni.
Wito huo umetolewa na Katibu Tawala wa wilaya hiyo, Pendo Abdallah Mahalu, alipomwakilisha Mkuu wa wilaya hiyo katika mbio za Afya ya Mama Kigamboni City Mararhon, zilizoandaliwa na Taasisi ya Afya ya Mama Foundation kwa lengo la kukusanya kiasi hicho cha fedha.
Mbio hizo zilizoanzia katika viwanja vya Tungi Mnadani, Daraja la Nyerere, wilayani Kigamboni, mkoani Dar es Salaam, zilihusisha wakimbiaji kutoka Club mbalimbali za marathon nchini kwa umbali wa kilometa tano na kilometa 21.
Pendo ameeleza harambee hiyo muhimu ina lenga kukusanya fedha kiasi cha sh. milini 105, zitakazo saidia ununuzi wa vifaa tiba vikiwamo mashine za kupima na kuangalia ishara ya uzima wa mtoto, vifaa vya kusaidia upumuaji wa mtoto mchanga na zana za kupima kiwango cha Oksjeni katika damu.
"Pia zinahitaji seti maalumu za vifaa safi na salama vya kujifungulia kwaajili ya wajawazito, vitanda vya kujifungulia na vifaa vya wodi ya uzazi,"amesema Pendo.
Amesema serikali chini ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, inaendelea kuwekeza kwa kasi kubwa katika sekta ya afya kwa kujenga zahanati, vituo vya afya na hospitali za wilaya kote nchini ingawa ushiriki wa wadau bado unahitajika.
"Ninaipongeza taasisi hii isyo ya kiserikali ya Afya ya Mama Foundation kwa kuandaa mbio hizi ili kukamilisha pale penye mapungudu na kukuhakikisha huduma zinawafikia walengwa,"amesema Pendo.
Ameomba wadau kusaidia kufanikisha harambee hiyo muhimu yenye lengo la kuboresha huduma za adya wilayani Kigamboni.
Mwenyekiti wa Bodi ya Afya ya Mama Foundation, Felister Bwana, amesema taasisi hiyo iliasisiwa kwa lengo kuu la kuhakikisha hakuna mama anayepoteza maisha waati wa kujifungua.
"Katika kufuatilia huduma za afya ya uzazi Wilaya ya Kigamboni, taasisi ilibaini kuwa vituo vyetu vya afya na zahanati bado vinakabiliwa na uhaba wa vifaa tiba na miundombinu katika kutoa huduma za msingi kwa mama na watoto wachanga,"amesema Felister.
Ameongeza, changamoto hizo zimechangia kuandaa mbio hizo zenye kauli mbiu ya Mama Imara, Taifa Imara kwa lengo la kufanya harambee ya kukusanya kiasi cha Sh. milioni 105 kununua vifaa tiba.
Mkurugenzi wa Biashara wa Azania Bank, Yahaya Mbanka, amesema benki hiyo itachangia Sh. milioni 5 kufanikisha hatua hiyo.

.jpeg)
.jpeg)
.jpeg)