Celine Mollel Atwaa Taji la Miss Ilala 2026


Na MWANDISHI WETU

MREMBO Celine Mollel ametwaa taji la Miss Ilala 2026 katika fainali za mashindano hayo zilizofanyika katika ukumbi wa The Dreamer’s Lounge, Chanika, Wilaya ya Ilala, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.

Mashindano hayo yalishirikisha warembo 13 waliokuwa wakichuana kuwania taji hilo, ambapo Celine Mollel aliibuka mshindi wa kwanza, akifuatiwa na Hadija Azary aliyeshika nafasi ya pili, Irene Yoram nafasi ya tatu, Karen Angelo nafasi ya nne na Rosemary Galibona aliyeingia tano bora kwa kushika nafasi ya tano.

Akizungumza katika fainali hizo, Meya wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Nurudini Bilal, aliwapongeza waandaaji wa mashindano hayo kwa kufanikisha tukio hilo lililoshuhudia ushindani mkubwa miongoni mwa washiriki.

Bilal amesema Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, itaongeza nguvu katika kusaidia mashindano hayo mwaka ujao ili kuitangaza Ilala ndani na nje ya nchi.

Amesema warembo watakaofanya vizuri katika mashindano hayo watapata fursa ya kushiriki Miss Dar es Salaam na, kwa kufanya vizuri katika hatua zinazofuata, wanaweza kufikia mashindano ya Miss Tanzania.

Aidha, amesema mashindano hayo yana nafasi ya kuwafungulia warembo milango ya ajira na fursa mbalimbali za kiuchumi kupitia sekta ya urembo.

Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Chanika, Gaudence Kashoka, alisema Ilala ni miongoni mwa maeneo yanayochangia kwa kiwango kikubwa mapato ya Jiji la Dar es Salaam.

Amesema kupitia mashindano hayo, warembo watapata fursa ya kuitangaza Ilala pamoja na vivutio vyake vya utalii, jambo litakalosaidia kuongeza mwonekano wa eneo hilo na kuvutia wageni.

Mkurugenzi wa mashindano hayo, Lucas Rutainurwa, alisema zawadi zenye thamani ya Sh milioni 7.4 zilitolewa kwa washindi na washiriki.

Amesema mshindi wa kwanza alizawadiwa Sh milioni mbili, mshindi wa pili Sh milioni 1.5, mshindi wa tatu Sh milioni moja, mshindi wa nne Sh 800,000 na mshindi wa tano Sh 500,000.

Rutainurwa aliongeza kuwa washiriki wengine wanane ambao hawakufanikiwa kuingia tano bora walipatiwa kifuta jasho cha Sh 200,000 kila mmoja.

Naye Mratibu Mkuu wa mashindano hayo, Yasinta Mtayabarwa, alisema warembo waliopata tiketi ya kushiriki Miss Dar es Salaam wameanza maandalizi ya kujiandaa na hatua zinazofuata, ikiwamo kuingia kambini.

Mtayabarwa amesema Ilala imejipanga kuhakikisha warembo wake wanafanya vizuri katika mashindano yajayo na kuwania mataji mbalimbali.