Historia Yaandikwa Mnazi Bay, Waziri Homera Atangaza Ugunduzi wa Gesi Asilia wa Futi za Ujazo Bilionu 223


Mtwara

Waziri wa Nishati, Dkt. Juma Zuberi Homera, ametangaza rasmi ugunduzi mpya wa gesi asilia wenye kiasi cha futi za ujazo bilioni 223 katika Kitalu cha Mnazi Bay, mkoani Mtwara, kufuatia uchimbaji wa kisima cha utafiti cha Kasa-1X ST2.

Ugunduzi huo umefanywa na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kwa kushirikiana na kampuni ya Maurel & Prom (M&P), ukiwa ni ugunduzi mpya wa gesi asilia nchini baada ya zaidi ya miaka 10 tangu ugunduzi wa mwisho uliporipotiwa mwaka 2015.

Akizungumza katika hafla ya kutangaza ugunduzi huo iliyofanyika mkoani Mtwara, Waziri Homera amesema hatua hiyo ni muhimu katika kuimarisha upatikanaji wa nishati ya uhakika, kuongeza uzalishaji wa gesi asilia na kuchochea maendeleo ya uchumi wa Taifa.

Amesema ugunduzi huo unakuja wakati mahitaji ya nishati yakiongezeka kutokana na ukuaji wa viwanda na shughuli nyingine za kiuchumi, hivyo kuwa na umuhimu katika kuhakikisha nchi inapata nishati safi, salama, ya uhakika na inayopatikana kwa gharama himilivu.

Waziri Homera ameeleza kuwa kisima cha Kasa-1X ST2 kinatarajiwa kuzalisha takribani futi za ujazo milioni 30 za gesi asilia kwa siku kwa kipindi kisichopungua miaka 10.

Aidha, amesema visima vingine viwili vya MB-5 na MS-2 vilivyochorongwa katika Kitalu cha Mnazi Bay vimeongeza uzalishaji kwa zaidi ya futi za ujazo milioni 65 kwa siku.

Gesi Kuimarisha Usalama wa Nishati na Uzalishaji wa Umeme

Amesema zaidi ya asilimia 80 ya gesi asilia inayozalishwa katika Kitalu cha Mnazi Bay hutumika kuzalisha umeme kupitia mitambo ya TANESCO iliyopo Mtwara na Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa Waziri, ongezeko la uzalishaji wa gesi linatarajiwa kuimarisha usalama wa nishati nchini na kupunguza utegemezi wa nishati inayoagizwa kutoka nje, ambayo bei na upatikanaji wake huathiriwa na mabadiliko ya soko la kimataifa na migogoro ya kisiasa.

Kuongeza Mapato ya Serikali na Kukuza Uchumi

Homera amesema ugunduzi huo unatarajiwa kuongeza mapato ya Serikali kupitia mgawo wa gesi ya faida kwa mujibu wa Mkataba wa Ugawanaji wa Mapato ya Petroli (PSA), mapato ya TPDC kama mbia na kodi mbalimbali.

Vilevile, shughuli za kiuchumi zinazohusiana na mradi zinatarajiwa kuchangia kuongeza mapato ya Halmashauri za Mkoa wa Mtwara, kupunguza gharama za nishati kwa viwanda na kaya, pamoja na kuchochea ukuaji wa viwanda nchini.

Ameongeza kuwa gesi asilia inaweza kutumika kama malighafi katika uzalishaji wa bidhaa za petrokemikali, zikiwemo plastiki na mbolea, hatua inayoweza kuongeza thamani ya rasilimali za ndani na kusaidia sekta nyingine za uzalishaji.

TPDC Yaongeza Ushiriki Wake Mnazi Bay

Akizungumzia ushiriki wa Serikali katika Kitalu cha Mnazi Bay, Waziri Homera amesema TPDC ilikuwa na hisa za asilimia 20 kabla ya kuongeza ushiriki wake hadi asilimia 40 mwaka 2024 kupitia ununuzi wa hisa.

Amesema ongezeko hilo limeimarisha ushiriki wa Serikali katika maamuzi ya kimkakati kuhusu uendelezaji wa kitalu hicho na kuongeza fursa za mapato yatokanayo na uzalishaji wa gesi asilia.

Miradi ya LNG na Fursa za Uwekezaji

Homera amesema ugunduzi huo unatarajiwa kuimarisha imani ya wawekezaji na kuvutia mitaji zaidi kutoka ndani na nje ya nchi.

Katika hatua nyingine, amesema TPDC imeingia katika majadiliano na wawekezaji wanne wanaopanga kuendeleza miradi midogo ya gesi asilia kimiminika (LNG), ambapo miradi mitatu inatarajiwa kutekelezwa mkoani Mtwara.

Amesema miradi hiyo inatarajiwa kuongeza ajira, kupanua matumizi ya gesi asilia na kuwezesha matumizi yake katika magari kama mbadala wa petroli na dizeli.

Watanzania Wanufaika na Ajira na Zabuni

Kwa mujibu wa Homera, takribani Watanzania 200 wameajiriwa katika shughuli mbalimbali kupitia kampuni za kizawa, huku zabuni 35 zenye thamani ya zaidi ya Shilingi bilioni 20 zikitolewa kwa wazawa.

Aidha, amesema asilimia 95 ya waajiriwa katika shughuli za uzalishaji na uchakataji wa gesi ni Watanzania, huku Kiwanda cha Kuchakata Gesi cha Madimba kikiendeshwa kwa asilimia 100 na Watanzania.

Amesema hatua hizo zinaimarisha ushiriki wa wazawa katika sekta ya mafuta na gesi, uhamishaji wa ujuzi na kujenga uwezo wa kitaifa katika shughuli za utafutaji, uzalishaji na uchakataji wa rasilimali hizo.

Wananchi Kunufaika na Miradi ya Kijamii

Homera ameeleza kuwa wananchi wa Mtwara na maeneo jirani wameendelea kunufaika na miradi ya kijamii inayotekelezwa na TPDC kwa kushirikiana na Maurel & Prom, ikiwemo miradi ya elimu, afya, uhifadhi wa mazingira, uwezeshaji wa wanawake na ufadhili wa masomo kwa wanafunzi.

Amewapongeza TPDC, Maurel & Prom na wataalamu wote walioshiriki katika kufanikisha uchimbaji wa kisima cha Kasa-1X ST2 na ugunduzi huo, akisisitiza umuhimu wa kuendeleza rasilimali za mafuta na gesi kwa manufaa ya Taifa.