Na MWANDISHI WETU, Dodoma
JESHI la Polisi Tanzania limesema silaha haramu 230, zimesalimishwa na wananchi kwa hiari katika kipindi cha kuanzia Septemba Mosi hadi Oktoba 19, 2026, huku likiwataka wanaomiliki silaha hizo kuzisalimisha kabla ya muda wa msamaha kumalizika Oktoba 31, mwaka huu.
Kwa mujibu wa taarifa kwa umma iliyotolewa na Msemaji wa Jeshi la Polisi, David Misime katika Makao Makuu ya Jeshi la Polisi jijini Dodoma, Oktoba 20, 2026, silaha zilizokabidhiwa ni pamoja na magobole 150, shotgun 50, rifle 15, bastola nane, AK-47 tano na Mk IV mbili.
Jeshi hilo limesema kampeni hiyo ya kitaifa ilizinduliwa Agosti 31, 2026, na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Patrobas Paschal Katambi, jijini Dodoma, kufuatia Tangazo la Serikali Na. 251 la Agosti 28, 2026, lililotangaza msamaha kwa wamiliki wa silaha haramu watakaokabidhi silaha hizo ndani ya muda uliopangwa.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, wananchi wanaotaka kusalimisha silaha wanatakiwa kufanya hivyo kuanzia saa mbili asubuhi hadi saa kumi jioni kila siku katika vituo vya polisi, ofisi za serikali za mitaa au vijiji na ofisi za watendaji wa kata au shehia.
Silaha zinazotakiwa kusalimishwa ni zile zinazomilikiwa bila vibali na ambazo hazijawahi kusajiliwa nchini, zikiwamo bastola, shotgun, rifle, magobole na silaha za kijeshi. Pia, kampeni hiyo inahusu silaha zilizokuwa zinamilikiwa kihalali na watu waliofariki, lakini ndugu zao wakaendelea kuzihifadhi nyumbani badala ya kuzipeleka polisi kuhifadhiwa wakati taratibu za mirathi zikiendelea.
Jeshi la Polisi limeonya kuanzia Novemba Mosi, 2026, litafanya misako nchi nzima kwa lengo la kuwakamata na kuwachukulia hatua za kisheria watu watakaobainika kuendelea kumiliki silaha haramu baada ya kushindwa kutumia fursa ya msamaha.
Taarifa hiyo imeeleza kifungu cha 62 cha Sheria ya Udhibiti wa Silaha na Risasi, Sura ya 223, marejeo ya mwaka 2023, kinaweka adhabu ya kifungo cha miaka 10 jela au faini ya Sh milioni 15, au adhabu zote mbili kwa pamoja, kwa mtu atakayepatikana na hatia ya kumiliki silaha kinyume cha sheria.
Jeshi hilo limetolea mfano vipindi vya awali vya msamaha, kuanzia Novemba 2023 hadi Agosti 2024, kulikuwa na kesi 165 zilizohusu kupatikana na silaha kinyume cha sheria, huku washitakiwa 176 wakikamatwa na kufikishwa mahakamani. Katika kipindi cha Novemba 2024 hadi Agosti 2025, kesi 158 ziliripotiwa na washitakiwa 161 wakakamatwa na kufikishwa mahakamani.
Aidha, katika kipindi cha Novemba 2025 hadi Agosti 2026, taarifa hiyo imesema kulikuwa na kesi 183 za makosa ya kumiliki silaha kinyume cha sheria, huku washitakiwa 172 wakikamatwa na kufikishwa mahakamani.
Katika hatua nyingine, Jeshi la Polisi limewahimiza wananchi wanaomiliki silaha kihalali lakini wanakabiliwa na changamoto za kiafya, umri mkubwa au hali nyingine zinazoweza kuwafanya washindwe kuzitunza kwa umakini unaotakiwa kisheria, kuzisalimisha ili kuzuia zisiangukie mikononi mwa watu wasiostahili.
Vilevile, wamiliki wa silaha halali wametakiwa kufika katika vituo vya polisi vya wilaya, uhakiki wa silaha zao, wakiwa na silaha husika, leseni na picha moja ya pasipoti.
Jeshi la Polisi limewasihi wananchi kutumia siku zilizobaki za msamaha kusalimisha silaha haramu kwa hiari ili kuepuka kukamatwa na kuchukuliwa hatua za kisheria baada ya muda huo kumalizika.
