Na MWANDISHI WETU
Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), imetangaza Awamu ya Kwanza ya upangaji mikopo na ruzuku kwa wanafunzi 165,775 yenye thamani ya Sh. bilioni 535.7.
Akizungumza na waandishi wa habari, Dar es Salaam, Oktoba 10, 2026, Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Dk. Bill Kiwia, alisema fedha hizo ni kugharimia wanafunzi wa stashahada, shahada ya awali, wanaoendelea na masomo na wanaofadhiliwa kupitia Samia Scholarship, waliodahiliwa katika vyuo mbalimbali kwa mwaka wa masomo 2026/2027.
Dk. Kiwia ametaja idadi ya wanufaika wa mwaka wa kwanza na kiasi cha fedha kuwa ni Wanafunzi 74,769 wa shahada ya awali wamepangiwa mikopo (Sh. Bilioni 246.88), Wanafunzi 8,538 wa stashahada (Sh. 22.9 bilioni) na Wanafunzi 873 wa Samia Scholarship waliopangiwa ruzuku kiasi cha 4.5 bilioni.
Aidha, Dk. Kiwia amesema kwa wanufaika wanaoendelea na masomo ambapo Wanafunzi 79,115 wamepangiwa mkopo kiasi Sh. bilioni 252.4, Wanafunzi 1,554 wa stashahada wamepangiwa mikopo wa Bilioni 3.8 na Wanafunzi 926 wa Samia Scholarship, waliopangiwa ruzuku ya Sh. bilioni 5.1.
Pia amesema awamu ya pili ya waliopangiwa mikopo, HESLB inawakumbusha waombaji wa mikopo na ruzuku ambao hawakupangiwa mikopo au ruzuku katika awamu ya kwanza, kuendelea kufuatilia taarifa za maombi yao kupitia 'SIPA', wakati taratibu za uchambuzi na upangaii wa mikopo na ruzuku kwa mwaka 2026/2027 zikiendelea.
Dk. Kiwia ameongeza kwamba katika awamu ya kwanza HESLB imepanga Sh. bilioni 535.7 kwa wanafunzi 165,775, wakijumuisha wanafunzi wapya wa shahada ya kwanza, wanafunzi wa stashahada, wanufaika wa Samia Scholarship pamoja na wanafunzi wanaoendelea na masomo.
Amesema itakumbukwa Serikali imetenga Sh. trilioni 1.06 za mikopo na ruzuku ili kugharimia Wanafunzi 292,463, wakiwemo wanafunzi 111,342 wa mwaka wa kwanza na shahada ya awali.
Dk. Kiwia amesema Wanafunzi 24,978 wa Stashahada, wakiwemo wanafunzi 14,000 wa mwaka wa kwanza, Wanafunzi 2,738 wa shahada ya awali wanaofadhliwa kupitia Samia Scholarship, wakiwemo wanafunzi wapya 1,000 na Wanafunzi 513 wa Stashahada ya Juu ya Sheria kwa Vitendo wakiwemo wapya 350.
