Balozi Mulamula - Uwekezaji kwa Wanawake ni Msingi Maendeleo na Udhibiti Ndoa za Utotoni


Na MWANDISHI WETU

Mjumbe Maalumu wa Umoja wa Afrika anayeshughulikia masuala ya Wanawake, Amani na Usalama, Balozi Liberata Mulamula, amesema uwekezaji kwa wanawake na watoto wa kike kupitia elimu na uchumi ni msingi muhimu wa kuleta mabadiliko chanya kwa jamii.

Akizungumza katika jukwaa la The Power Table 2026, lililofanyika Dar es Salaam katika Ubalozi wa Afrika ya Kusini, likiwa na kauli mbiu isemayo "Nguvu ya Mtoto wa kike, Komesha ndoa za utotoni, Wekeza katika haki za wasichana".

Balozi Mulamula amesisitiza umuhimu wa kuwapa wanawake nafasi ya kushiriki katika uongozi na michakato ya kufanya maamuzi, akibainisha kuwa Tanzania imepiga hatua kubwa katika eneo hilo.

Ametolea mfano uongozi wa Rais wa kwanza mwanamke wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, akisema hatua hiyo ni ushahidi kuwa wanawake wana uwezo wa kuongoza na kuleta mabadiliko yanayoonekana.

Pia, amesema uwekezaji wa kielimu na kulinda haki za wanawake ndani jamii, itasaidia kuepusha ndoa za utotoni ambazo zinaharibu mustakabali wanafunzi wa kike kufikia ndoto zao.

Kwa upande wake, Balozi wa Afrika Kusini nchini Tanzania, Noluthando Mayende-Malepe, amesema jukwaa hilo limebeba ajenda muhimu ya Maendeleo ya wanawake na wasichana, katika kulinda haki zao, kutambua umuhimu wa uwezeshaji kiuchumi kwa wanawake na ushirikishwaji katika maamuzi ya familia.

Jukwaa hilo limewakutanisha wanawake kubadilishana mawazo, uzoefu na mitazamo kuhusu uongozi jumuishi, huku likisisitiza umuhimu wa kuhakikisha sauti za wanawake zinasikika na mchango wao unazingatiwa katika maamuzi yanayoathiri jamii.

Kupitia ujumbe wa washiriki, jukwaa hilo pia limeendelea kuhamasisha wanawake kujifunza kutoka kwa viongozi wenye uzoefu, kujenga uwezo na kutumia nafasi zilizopo kuleta mabadiliko chanya.