Na MWANDISHI WETU
WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi, Dk. Bashiru Ally, amesema serikali imeweka mkakati wa kuleta mapinduzi makubwa katika sekta za mifugo na uvuvi nchini, inayolenga kuongeza tija, kuzuia upotevu wa mazao na kuimarisha uchumi wa taifa kuelekea Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050.
Akizungumza katika uzinduzi wa maabara mpya ya utafiti wa ongezeko la asidi baharini na athari zake kwa viumbe hai ya Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI), Kunduchi, Dar es Salaam.
Dk. Bashiru amesema maabara hiyo itasaidia kuendesha shughuli za uvuvi na mifugo kisayansi, kuwekeza katika utafiti na kujenga uwezo wa wanasayansi, kupata matokeo yanayotarajiwa na kuleta tija kwa taifa.
Amesema sekta ya uvuvi ni nguzo muhimu kwa uchumi na ustawi wa jamii kwani takriban Watanzania milioni saba wanategemea sekta hiyo kwa ajira na maisha yao kwa ujumla.
Amesema sekta hiyo ni chanzo kikubwa cha protini, lishe bora na usalama wa chakula nchini, lakini taifa halijanufaika nayo vya kutosha kutokana na uduni katika maeneo ya utafiti, mafunzo na uwekezaji.
Pia, Dk. Bashiru amesema serikali imeingia mikataba ya kununua wa meli sita za uvuvi za kisasa tatu Zanzibar na tatu Bara, kuwezesha Watanzania kuvua wenyewe badala ya kutegemea kukodisha na kukusanya tozo pekee.
Amesema kukamilika kwa ujenzi wa Bandari ya Uvuvi ya Kilwa, ambayo hivi sasa inasubiri uzinduzi rasmi na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, bandari hiyo imesheheni miundombinu ya kisasa ikiwemo vyumba vya ubaridi, viwanda vya uchakataji na mifumo ya kuzuia upotevu wa samaki unaofikia asilimia 30 hivi sasa.
Kwa upande wa Mkurugenzi Mkuu wa TAFIRI, Dk. Ismael Kimirei, amesema uwepo wa maabara hiyo ni hatua inayolenga kuwasaidia wavuvi na wakulima wa viumbe maji kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Amesema ongezeko la asidi baharini linatokana na kuongezeka kwa hewa ya ukaa inayozalishwa kwa kiasi kikubwa na shughuli za binadamu.
Dk. Kimirei amesema hata ongezeko dogo la asidi baharini lina madhara makubwa kwa viumbe maji, ikiwemo kuyeyuka kwa miamba ya matumbawe badala ya kukua kwa kuongeza madini ya calcium carbonate.
Amesema kutoweka kwa miamba hiyo kunahatarisha ulinzi wa asili wa maeneo ya nchi kavu, kwani mifumo ikolojia ya baharini inategemeana katika kupunguza nguvu ya mawimbi makubwa yanayotokana na majanga ya kimbunga au tsunami.
"Nguvu ya wimbi kubwa inapunguzwa katika awamu tatu; awamu ya kwanza ambayo ni ngao ya msingi ni mwamba wa matumbawe hai, ikifuatiwa na mfumo wa pili wa nyasi bahari, na awamu ya tatu ni miti ya mikoko. Maeneo yenye muunganiko wa mifumo hii mitatu yanakuwa salama zaidi kwa watu wanaoishi nchi kavu," amesema.
Mkurugenzi Mkuu huyo amesema kupitia maabara hiyo mpya, TAFIRI itafanya tafiti za kina kubaini aina ya viumbe maji na mimea ya baharini inayoweza kuhimili ongezeko la asidi, kupanda kwa joto pamoja na pungufu wa oksijeni.
Amesema matokeo ya tafiti hizo yatatumika kuishauri Serikali na kuwaelekeza wananchi wanaojishughulisha na uvuvi, kilimo na ufugaji wa viumbe maji kama vile kaa, kamba mti, chaza na mwani ili wachague aina zinazohimili mabadiliko hayo badala ya kuendelea kupata hasara.
Aidha, Dk. Kimirei ameongeza kuwa TAFIRI kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) inaendelea na mradi wa urejesho wa nyasi bahari katika maeneo ya Kigamboni jijini Dar es Salaam na Chongoleani na mkoani Tanga.
Amesema Katika mradi huo, wananchi wamefundishwa mbinu za kurejesha nyasi hizo ili ziendelee kutekeleza jukumu lake la asili la kushyonza na kupunguza makali ya asidi baharini.