Katibu Tawala Igunga Apongeza Uamuzi wa Rais Dk. Samia Kuanzisha NAESA Kuimarisha Huduma za Ugani


KATIBU Tawala wa Wilaya ya Igunga Mkoani Tabora, Elizabeth Rwegasira amemshukuru Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kuunda Taasisi ya Wakala wa Taifa ya Huduma za Ugani (NAESA), ili kuongeza nguvu na rasilimali kwenye kilimo kiendelee kuwa na tija.

Elizabeth ametoa shukrani hizo wakati alipopokea Viongozi kutoka katika Taasisi hiyo mpya (NAESA), walipofika kuitambulisha katika Ofisi ya  Katibu Tawala wa Wilaya hiyo mjini Igunga.

‘’Licha yakuwa kuna mambo mengine lakini Kilimo ndio kila kitu katika maisha yetu ya kila siku, hivyo tunampongeza Rais kwa maamuzi yake haya na sisi tupo tayari kupokea maboresho haya,’’ amesema.

Kwa upande wa Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Ufuatiliaji wa Tathmini Wakala wa Taifa ya Huduma za Ugani (NAESA), Paul Katemi amesema Wakala hiyo ni mpya imeundwa kutoka Wizara ya Kilimo ambayo ilizinduliwa na Rais Dk. Samia.

Amesema Wakala hiyo inamalengo kuwahamisha Maofisa Ugani nchini kuhamia NAESA kwa lengo la kuhakikisha inawasimamia vema kuongeza uzalishaji na tija kwenye kilimo.