JKCI Yapokea Kifaa cha Kisasa cha Kufungua Kifua Wakati wa Upasuaji wa Moyo Kutoka GSM Foundation


Na MWANDISHI WETU

TAASISI ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), imepokea kifaa cha kisasa kinachotumika kufungua kifua wakati wa upasuaji wa moyo kwa wototo na watu wazima kutoka kwa Foundation ya GSM chenye thamani ya sh.milioni 50 kinachojulikana kama Sternal Saw.

Akizungumza wakati wa kupokea kifaa hicho, Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Dk.Peter Kisenge,  alisema kitasaidia kuboresha utoaji huduma hizo kwa watoto na watu wazima katika ubora mkubwa na kwa watu wengi zaidi.

"Tunayofuraha na tunawashukuru ndugu zetu wa GSM Foundation, kwani wametupatia kifaa kinachotumika kufungua kifua wakati wa upasuaji wa moyo kijulikanacho kama Sternal saw, hatua hii ni sehemu muhimu yenye dhamira njema ya kuunga mkono jitihada za Rais Dk.Samia Suluhu Hassan za kuboresha huduma za upasuaji wa moyo na kuokoa maisha ya wananchi,"alisema.

Alieleza kuwa, GSM Foundation ni wadau wakubwa wa JKCI, katika kutekeleza majukumu yao ya utoaji huduma za upasuaji kwa wananchi, kwani wamekuwa msaada mkubwa na kutoa ushirikiano wa karibu katika kutekeleza Dk.Samia Tiba Mkoba kwa wananchi wa mikoa mbalimbali na kusaidia gharama za upasuaji wa moyo kwa watoto 50, hivyo wataendelea kushirikiana nao.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya GSM Foundation, Faith Gugu, alisema JKCI ni mdau muhimu katika kuokoa maisha ya wananchi kupitia matibabu ya moyo, ndiyo maana wameguswa kutoa kifaa hicho chenye tija kubwa katika huduma hizo.

Aliwapongeza kwa jitihada kubwa wanazozifanya na kuahidi ushirikiano zaidi wakati wowote kuhakikisha wananchi wanapata huduma njema na kuokoa maisha ya wananchi.

Ofisa Muuguzi anayetoa huduma katika chumba cha upasuaji wa moyo JKCI, Hania Bhahama, aliishukuru GSM, kwani kifaa hicho kitasaidia kwa sehemu kubwa kutoa huduma bora na kwa watu wengi zaidi.