Na MWANDISHI WETU
Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dk. Asha-Rose Migiro, amechaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa Uongozi wa Umoja wa Vyama vya Siasa Barani Afrika (APPI) kwa Kanda ya Afrika Mashariki.
Taarifa iliyotolewa na Katibu wa NEC ya CCM, Itikadi, Uenezi na Mafunzo, imeeleza kuwa uchaguzi huo ulifanyika katika Mkutano wa Pili wa Vyama vya Siasa Barani Afrika (African Political Parties Summit), uliofanyika jijini Addis Ababa, Ethiopia, kuanzia tarehe 5 hadi 7 Novemba 2026.
Mkutano huo uliwakutanisha viongozi wa vyama vya siasa kutoka nchi mbalimbali barani Afrika, ambapo walijadili nafasi ya vyama hivyo katika kuimarisha utawala, ushirikiano wa kisiasa na mageuzi ya kiuchumi.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, CCM iliwakilishwa na Naibu Katibu Mkuu wa CCM Bara, Aggrey Mwanri, pia alishiriki majadiliano kuhusu kuimarisha demokrasia na mshikamano barani Afrika.
Aidha, mkutano huo umepitisha Hati ya Uanzishwaji na Uendeshaji wa APPI na kuridhia uongozi wake wa kwanza wenye wajumbe 17, utakaoongozwa na Mwenyekiti wa Chama tawala cha National Democratic Congress (NDC) cha Ghana, Johnson Asiedu Nketiah.
Katika taarifa hiyo imeeleza kuwa CCM imepokea kwa heshima na shukrani dhamana hiyo ya uongozi, ambayo inatoa fursa ya kuendelea kuchangia katika kuimarisha mshikamano na kubadilishana uzoefu baina ya vyama vya siasa barani Afrika.
Mkutano huo pia umepitisha Azimio la Addis Ababa, linalosisitiza wajibu wa vyama vya siasa katika kuimarisha taasisi za kidemokrasia, utawala bora, uwekezaji wenye tija, maendeleo ya viwanda, biashara baina ya nchi za Afrika na upatikanaji wa fursa za ajira, hususan kwa vijana na wanawake.
Vilevile, taaria hiyo imeeleza kuwa mkutano umekubaliana kuanzisha Baraza la Shule na Taasisi za Vyama vya Siasa Barani Afrika (CAPPSI) na Chuo cha Uongozi wa Mageuzi (PAT L) kwa lengo la kuimarisha elimu ya siasa na uongozi.
Pia mkutano huo umekubaliana kuanzisha mashauriano ya kuandaa ajenda ya APPI 2040, itakayosaidia kuelekeza ushirikiano wa vyama vya siasa katika kufanikisha vipaumbele vya maendeleo ya Afrika na Ajenda ya Umoja wa Afrika ya 2063.
CCM imesisitiza kuwa itaendelea kushirikiana na vyama vingine vya siasa barani Afrika katika kuimarisha taasisi za kisiasa na kuchangia utekelezaji wa ajenda za maendeleo kwa ustawi wa wanachi.
