HearWell Audiology Yaongoza Kukuza Afya ya Masikio na Usikivu Shule ya Viziwi ya Msandaka, Moshi


Na MWANDISHI WETU

HearWell Audiology Clinic imeendelea kuonesha mchango wake katika kukuza afya ya masikio na usikivu nchini kupitia ushiriki wake katika kambi maalumu ya uchunguzi wa afya ya masikio na usikivu iliyofanyika katika Shule ya Viziwi ya Msandaka, Moshi.

Kambi hiyo ya uchunguzi ilikuwa sehemu ya shughuli za kijamii zilizoandaliwa katika Kongamano la Mwaka la Jumuiya ya Madaktari Bingwa wa Magonjwa ya Masikio, Pua na Koo Tanzania (TENTS), lililofanyika Moshi kuanzia Novemba  4 hadi 7, 2026.

Akizungumzia kambi hiyo, Mtaalam wa usikivu ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa HearWell Audiology Clinic, Fayaz Jaffer, amesema wamelenga kuwafikia wanafunzi 74 wenye umri wa miaka 6 hadi 16 pamoja na wafanyakazi 23 wa shule hiyo.

 Amesema kambi hiyo imejumuisha wataalamu wa HearWell Audiology Clinic na timu ya madaktari kutoka Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kilimanjaro (KCMC) kwa ajili ya kufanya uchunguzi wa masikio na vipimo vya usikivu.

Jaffer amesema kwa kushirikiana na Rashida Hassuji, mtaalamu wa usikivu (Audiologist) wa HearWell, walifanya vipimo vya usikivu kubaini wenye changamoto za kusikia ambao wanaweza kunufaika na uchunguzi zaidi, huduma za urekebishaji wa usikivu na vifaa saidizi vya kusikia (hearing aids).

Pia, Mkurugenzi Jaffer, alitoa wito kwa madaktari bingwa wa ENT kuanzisha kambi za uchunguzi katika mikoa yao na kuzifanya sehemu ya kalenda zao za shughuli za kila mwaka.

Kwa upande wake, Rashida Hassuji ameeleza kuwa katika uchunguzi huo watoto kadhaa walibainika kuwa na matatizo ya kuziba kwa masikio kutokana na mlundikano wa nta, uwepo wa vitu vya kigeni ndani ya masikio pamoja na maambukizi. Matatizo hayo yalishughulikiwa au kutibiwa wakati wa kambi, huku waliohitaji huduma zaidi za kibingwa wakipewa rufaa kwenda KCMC. 

Hassuji amesema uchunguzi wa mara kwa mara ni muhimu kwa watoto wenye changamoto za usikivu ili kutambua na kutibu matatizo mengine yanayoweza kuathiri zaidi uwezo wao wa kusikia. Utambuzi wa mapema husaidia kuboresha mawasiliano, ujifunzaji na ubora wa maisha.

Rais wa TENTS, Dk. Edwin Liyombo, amewashukuru wataalamu kutoka HearWell na KCMC kuandaa na kufanikisha zoezi hilo. Naye Mkuu wa Shule ya Viziwi ya Msandaka, Rossada Shao, ametoa shukrani kwa waandaaji na kusisitiza umuhimu wa uchunguzi huo, akiwaomba wataalamu hao kuzingatia kuendesha kambi kama hizo angalau mara mbili kwa mwaka. 

HearWell Audiology Clinic imekuwa ikishirikiana kwa karibu na taasisi mbalimbali za afya nchini, ikiwemo hospitali za serikali kama Muhimbili, katika kuendeleza na kutoa huduma za kibingwa. Kupitia ushirikiano na taasisi kama TENTS na KCMC, HearWell inaendelea kutekeleza dhamira yake ya kupeleka huduma karibu na wananchi, kuelimisha jamii na kuhakikisha watu wenye changamoto za usikivu wanapata huduma kwa wakati. Kwa HearWell, huduma bora za usikivu ni zaidi ya kutoa vifaa vya kusaidia kusikia; ni kuboresha mawasiliano, kuimarisha elimu na kuboresha maisha ya watu.