TAASISI ya Maendeleo ya Mkoa wa Kagera (KADEFO), inawakaribisha wanachama wake kuendelea kujisajili, kushiriki Mkutano Mkuu wa Kwanza unaotarajiwa kufanyika mkoani humo, Desemba 23, mwaka huu.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa KADEFO, Balozi Liberata Mulamula, mkutano huo utafanyika mkoani humo, Bukoba Mjini katika Ukumbi wa Mikutano wa Hoteli ya Bukoba Kolping na mgeni rasmi atakuwa Waziri wa Maliasili na Utalii Dk. Ashatu Kijaji, ambaye ni Mlezi wa Mkoa huo wa Kagera.
"Ninayofuraha kuwakaribisha wanachama wote katika Mkutano wetu huu muhimu wa kwanza tangu kusajiliwa rasmi kwa KADEFO. Pia, tunawakaribisha wanachama wapya kufika kujiunga na taasisi hii muhimu ya Maendeleo ya mkoa wetu wa Kagera,"alisema.
Alisema Maendeleo ya Mkoa wa Kagera yanajengwa na wanakagera wenyewe, hivyo ndiyo maana wanaendelea kuhimiza ushiriki wa wanachama wote na wale wapya kufika Ili kushiriki na kujadili pamoja agenda mbalimbali za maendeleo.
"Mkoa wetu wa Kagera umejaaliwa kuwa na fursa nyingi ikiwemo utalii, vyanzo mbalimbali vya nishati ya umeme ikiwemo maporomoko ya maji, fukwe nzuri, fursa ya kuzalisha hewa ukaa. Pia, tunayo mazao mengi ambayo ni kahawa, ndizi, mihogo na mengineyo, yanayoweza kuzalisha utajiri kwa wanakagera,"alisema.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi, Mama Illuminata Maerere, alisema maandalizi yanafanyika vizuri huku akisisitiza wanachama kuendelea kufanya usajili kufanikisha zoezi hilo muhimu.
