Balozi Mulamula-Mkutano wa Wabunge Wanawake Kichocheo cha Wanawake Kushiriki Kuleta Amani na Usalama Kanda ya Maziwa Makuu


Na MWANDISHI WETU

Mjumbe Maalumu wa Umoja wa Afrika(AU) kuhusu Wanawake, Amani na Usalama, Balozi Liberata Mulamula, amesema Mkutano wa Kimataifa wa Wabunge Wanawake wa Ukanda wa Waziwa Makuu (FP-ICGLR) ni sehemu muhimu ya kuhamasisha wanawake kushiriki kuleta amani na usalama katika ukanda huo na Afrika.

Balozi Mulamula ameyasema hayo Jijini Dar es Salaam, aliposhiriki mdahalo ikiwa sehemu ya mkutano huo, uliofanyika katika  Kituo cha Kimataifa wa Mikutano Julius Nyerere (JNICC).

"Mkutano huu ni wa aina yake ambao unakutanisha Wabunge, Maspika na wadau mbalimbali kujadili masuala ya msingi kuhusu ushiriki wa wanawake katika kuleta amani, usalama na maendeleo endelevu katika Kanda ya Maziwa Makuu.

Pia, utahamasisha wanawake kushiriki katika nafasi za uongozi kwa ngazi zote kwani asilimia yao ya ushiriki katika nafasi hizo na zile za maamuzi bado ni ndogo sana, hivyo Mkutano huu utaongeza chachu zaidi kwao,"amesema.

Ameeleza kuwa, Tanzania kuwa mwenyeji wa Mkutano huo ni heshima kubwa kwa Taifa na kutambua uongozi imara wa Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan.

"Tija kubwa ya kufanyika mkutano huo nchini ni kuuhakikishia ulimwengu kwamba Tanzania ni salama na imefungua milango kwa wote katika kuhamasisha diplomasia ya Ubunge( Parliamentary Diplomacy) na kukuza utalii,"amesema.

Balozi Mulamula amesema matokeo ya Mkutano huo yataonekana pale Azimio la Mkutano huo na yale ya mikutano ya nyuma yatakapotekelezwa kikamilifu na Mabunge kufuatilia utekelezaji wake kuhakikisha serikali zinawajibika kutenga bajeti stahiki na sera zenye kulenga kumuinua mwanamke na kumwezesha kushiriki kikamilifu kwenye nafasi za uongozi na maamuzi ya kuleta au kudumisha amani na usalama kwa jamii na nchi hizo.