Diwani Sharik Atoa Wito kwa Jamii Kuenzi Urithi wa Baba wa Taifa


Na MWANDISHI WETU

DIWANI wa Kata ya Kivukoni, maarufu kwa jina la 'Mtoto wa Kivukoni', Sharik Choughule, ameitaka jamii kuenzi na kuendeleza misingi na maono yaliyoachwa na Baba wa Taifa, Rais wa Kwanza wa Tanzania, Hayati Mwalimu Julius Nyerere.

Sharik ametoa wito huo Oktoba 14, 2026, jijini Dar es Salaam, baada ya kushiriki na kumaliza mbio za Tanzania–China Nyerere Run Marathon, zilizoandaliwa katika kuadhimisha kumbukizi ya  Baba wa Taifa.

Pia Sharik amekabidhi medali yake kwa mwananchi mwenye ulemavu, ikiwa ni ishara ya upendo, heshima na kuthamini mchango wa watu wenye ulemavu katika jamii.

Sharik amesema kitendo cha kumkabidhi medali mwananchi mwenye ulemavu kimeonesha umuhimu wa kujenga jamii inayojali, kuthamini na kuwajumuisha watu wote bila ubaguzi, kwa kuzingatia utu na usawa.

Akizungumzia umuhimu wa kuenzi urithi wa Mwalimu Nyerere, Shariki amesema Baba wa Taifa aliwaachia Watanzania tunu muhimu za amani, upendo, umoja na mshikamano, ambazo zinapaswa kulindwa na kuendelezwa na kila mwanajamii.

Sharik amesema jamii ina wajibu wa kuendeleza misingi hiyo kuhakikisha urithi wa Mwalimu Nyerere, unaendelea kuwa dira kwa vizazi vya sasa na vijavyo.

“Mwalimu Nyerere ametuachia amani na upendo. Hivyo, hatuna budi kuendeleza yote mema aliyotuachia, kwani huo ndio urithi wetu kama Watanzania”, alisema Sharik.