Standard Chartered Yachangia Sh. Milioni 21.4 Kuwaweza Wanawake kupitia Programu ya Mabinti ya CCBRT


Na MWANDISHI WETU

Benki ya Standard Chartered Tanzania imekabidhi mchango wa Sh. milioni 21.4 kwa Hospitali ya CCBRT, kusaidia programu ya kuwawezesha kiuchumi wanawake waliowahi kupata matatizo ya fistula.

​Msaada huo umetolewa kupitia taasisi ya benki hiyo (Standard Chartered Foundation), unalenga kutoa mafunzo ya ushonaji na usimamizi wa biashara na fedha kwa wanawake 40, kuwawezesha kujikwamua kiuchumi baada ya kukamilisha matibabu yao.

​Akizungumza wakati wa hafla ya makabidhiano hayo, Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya Standard Chartered Tanzania, Geofrey Mchangila, amesema mchango huo ni muendelezo wa jitihada za benki hiyo katika kuisaidia jamii.

​"Hii si mara ya kwanza kwetu kufanya hivi. Mapema mwaka huu, wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani, wafanyakazi wanawake wa benki yetu walishirikiana na mabinti wa programu hii na kuchangia cherehani 12 na kutoa elimu ya biashara na fedha," amesema Mchangila.

​Amesema msaada huo unakwenda sambamba na maadhimisho ya miaka 20 ya benki hiyo kimataifa katika kuleta mabadiliko chanya kwenye jamii. Mbali na mafunzo hayo, kila mwanamke atakayeshiriki anatarajiwa kupatiwa cherehani yake ili kuanza shughuli za uzalishaji mali.

​Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji Mkuu wa CCBRT, Brenda Msangi, ameishukuru benki hiyo kwa msaada huo uliotolewa kwa mara ya pili sasa.

​Brenda fedha hizo zitatumika kununulia vitendea kazi, ikiwemo cherehani, zitakazosaidia kuongeza wigo wa mradi wa Mabinti Centre. Mradi huo unalenga kuwajengea uwezo akina mama waliopona fistula kupitia mafunzo ya miezi minne.

​"Kuanzia Jumatatu hii, tunaanza darasa la pili kwa mwaka huu likiwa na wanawake 12. Lengo letu kuu ni kuwapa ujuzi na vitendea kazi vitakavyowawezesha kusimama wenyewe na kujipatia kipato pindi wanaporudi kwenye jamii zao," amesema Brenda.

​Amesema tangu kuanzishwa kwa programu hiyo, CCBRT imeshawawezesha zaidi ya wanawake 200 waliowahi kukumbwa na changamoto ya fistula.

​Pia, Brenda ametoa wito kwa wadau na mashirika mengine kujitokeza kuunga mkono jitihada hizo ili kuwafikia wanawake wengi zaidi waliopo kwenye dhiki na kuwarejeshea matumaini na utu wao katika jamii.