Na MWANDISHI WETU
UONGOZI mpya wa Taasisi ya Usanifu wa Kiswahili na Ushairi Tanzania (UKUTA) , umekabidhiwa rasmi ofisi kutoka kwa uongozi uliopita baada ya uchaguzi mkuu uliofanyika Julai 11 mwaka huu.
Akizungumza katika hafla ya makabidhiano hayo yaliyofanyika katika ukumbi wa Anatouglou, jijini Dar es Salaam, Makao Makuu ya UKUTA, Mwenyekiti wa taasisi hiyo taifa, Hussein Jimbika, amesema wamejipanga kusimamia kikamilifu usanifu wa lugha ya Kiswahili na ushairi nchini.
Amesema UKUTA itaendelea kuenzi jitihada kubwa za viongozi na waasisi wa taasisi hiyo, hususan Baba wa Taifa hayati Mwalimu Julius Nyerere, ambaye ndiyo mtu wa kwanza kuunda chombo hicho, kabla ya uhuru kwa kushirikiana na hayati Abeid Aman Karume na Sheikh Amri Abeid Karuta.
Ameeleza UKUTA ilitoa mchango mkubwa katika kufanikisha taifa kupata uhuru na kwamba uongozi wa taasisi hiyo utaendelea kufuata nyendo zao kuhakikisha safari ya kuenzi Kiswahili inafanikiwa.
“Wazee hawa walikuwa na makusudio makubwa ya Kiswahili kuwa ni nyenzo muhimu ya kupata uhuru na ustawi wa taifa", amesema.
Hivyo Uongozi mpya tutashirikiana na wenzetu kuhakikisha lengo la waasisi hawa linaendelewa na kufikiwa katika kukuza Kiswahili,”amesema Jimbika.
Jimbika amesema lengo lingine ni kuongeza usajili wa wanachama kwani mpaka sasa UKUTA inawachama 2050 tu.
Katibu Mkuu wa UKUTA, Abubakary Kiaibamba, amewarika wanachama katika ofisi za makao makuu ya taasisi hiyo zilizopo katika jengo la Anatouglou kwa uratibu wa shughuli zote za taasisi na kujisajili .
“Malengo yangu ni kuhakikisha tunakifanya Kiswahili kuwa bidhaa. Hii ndiyo kazi anayoifanya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan. Tutahakikisha vitabu vinaandikwa, mashairi yanatungwa na tunawakomboa washairi kiuchumi kupitia kazi zao,” amesema Kiaibamba.
Akikabidhi nyaraka za ofisi, Katibu Mkuu mstaafu Hassan Ligile, ameupongeza uongozi mpya kushinda katika uchaguzi wa kidemokrasia uliofanyika na kwamba wataendelea kutoa ushirikiano kuhakikisha UKUTA inasonga mbele huku akijivunia mafanikio yaliyopatikana chini ya uongozi wake.



