TAHAFE Yatangaza Kongamano la Hajj 2027, Yatoa Tahadhari Dhidi ya Matapeli


Na MWANDISHI WETU, Dar es Salaam

Shirikisho la Taasisi za Hijja Tanzania Bara (TAHAFE) limeandaa Kongamano na Maonesho ya Hajj 2027 na kuzitaka taasisi za hijja na mahujaji watarajiwa kukamilisha malipo ya maandalizi kwa wakati, kuepusha changamoto zinazotokana na ratiba mpya zilizowekwa na mamlaka za Saudi Arabia.

Akizungumza na waandishi wa Habari, Dar es Salaam, Julai 15, Naibu Katibu wa TAHAFE, Mahamed Mshangama, amesema kongamano hilo litafanyika Agosti 15, 2027 katika Ukumbi wa Lamada, Ilala, kwa lengo la kutoa elimu, mwongozo na kuonesha huduma zinazotolewa kwa mahujaji kupitia taasisi za hijja nchini Tanzania na Saudi Arabia.

 “Kongamano hilo litakuwa jukwaa muhimu kwa waumini wanaotarajia kutekeleza ibada ya Hijja mwaka 2027 kupata taarifa sahihi kuhusu taratibu za safari, huduma na maandalizi muhimu”, amesema.

Mshangama amesema kutokana na mabadiliko ya ratiba ya Wizara ya Hajj ya nchini Saudi Arabia, taasisi zote zinazosimamia mahujaji zinapaswa kuhakikisha zinakamilisha malipo ya gharama za maeneo ya malazi na mahema kabla ya Agosti 13, 2026, ambao ni mwisho wa muda uliowekwa na mamlaka za nchi hiyo.

 Amesema malipo ya mapema yatawezesha kuandaa  nafasi za mahujaji na kurahisisha maandalizi ya visa, hoteli na usafiri, hivyo mahujaji wanahimizwa kulipa gharama za Hijja mapema hata kwa utaratibu wa awamu.

Pia Mshangama amezitaja taasisi na mawakala walioidhinishwa kusafirisha mahujaji wa Tanzania Bara kwa mwaka 2027 kupitia mwavuli wa BITHA Bara na TAHAFE, ili kwalinda na matapeli.

Taasisi hizo ni Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA), Jamarat, Travel, Al Husna, Hajj Trust,  ZamZam, Rawdhwa, Masjid Adil, Kidunda, Ajwah, M2, Manasik, Musafir, Ahlubait, Nurpath.

 Mshangama amesema hatua hiyo inalenga kuwalinda wananchi dhidi ya matapeli wanaojifanya mawakala wa Hijja bila kuwa na kibali halali.

 Amesisitiza kuwa Idara Maalumu ya Kusimamia Hijja Tanzania (BITHA Bara) kwa kushirikiana na TAHAFE, ndiyo vyombo vyenye dhamana ya kuratibu, kusimamia na kuboresha huduma za mahujaji kutoka Tanzania wanaosafiri kwenda miji mitakatifu ya Makka na Madina.