Na MWANDISHI WETU
UANZISHAJI wa viwanda vya kuchakata na kuzalisha bidhaa za kilimo nchini Tanzania umeelezwa kuwa ni fursa muhimu ya kuwawezesha vijana kujiajiri, kuunda ajira na kuongeza thamani ya mazao ya ndani badala ya kutegemea kuuza malighafi nje ya nchi.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Plant Biodefenders, Dk. Never Mwambela, katika maadhimisho ya Wiki ya Ubunifu Tanzania na maonesho ya ubunifu yaliondaliwa na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) na Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), jijini Dar es Salaam, hivi karibuni.
Dk. Never amesema maonyesho hayo ni utekelezaji wa Ajenda ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050, ambayo kwa upande wa vijana inawalenga kuwa wasimamizi wa ujenzi wa viwanda na uanzishaji wa kampuni za Kitanzania zitakazosaidia kutengeneza ajira na kuwawezesha kujiajiri.
Amesema lengo ni kuhakikisha ifikapo mwaka 2050 vijana watakuwa wamejenga mifumo yao ya ajira kupitia kampuni wanazozianzisha na kuwa sehemu ya kukuza uchumi wao binafsi na uchumi wa taifa, badala ya kutegemea kutengenezewa au kupewa ajira.
Dk. Nwver amesema kwa sasa msukumo mkubwa umeelekezwa katika sayansi, teknolojia na TEHAMA, maeneo ambayo vijana wa kizazi cha sasa wana uwezo mkubwa, hususan katika matumizi ya teknolojia za kidijitali.
Amesema yeye ni mmoja wa wabunifu waliotokea katika vyuo vikuu nchini na kwamba kupitia tafiti alizofanya ameweza kuanzisha Kampuni ya Plant Biodefenders, ambayo imekuwa ikizalisha bidhaa za viuatilifu zenye tija kwa wakulima.
Dk. Never amesema miongoni mwa bidhaa zinazozalishwa na kampuni hiyo ni kiwatilifu kinacholenga kusaidia wakulima wa parachichi, hususan vijana wanaojishughulisha na kilimo hicho.
Amesema moja ya changamoto kubwa iliyokuwa ikiwakabili wakulima wa parachichi ni matumizi ya viwatilifu na mbolea za kemikali ambazo zinaweza kusababisha mazao kutokidhi mahitaji ya baadhi ya masoko ya Ulaya.
Kwa sababu hiyo, amesema vijana waliokuwa wamejiingiza katika kilimo cha parachichi walikabiliwa na changamoto ya kupata masoko ya nje kutokana na matumizi ya kemikali.
Dk. Never amesema suluhisho lililotengenezwa na Plant Biodefenders limewawezesha wakulima, hasa vijana, kulima kwa tija na kupata mavuno mengi ambayo ni salama kwao na kwa watumiaji, huku yakiwa na bei nzuri na soko la uhakika, hususan katika nchi za Ulaya.
Amesema kiwatilifu hicho kimesajiliwa hapa nchini kwa viwango vya kimataifa na kuthibitishwa, kuwa hakina mabaki ya sumu, jambo linalowezesha bidhaa zinazotokana na matumizi yake kuingia katika masoko mbalimbali ya dunia bila wasiwasi wa usalama wa bidhaa.
Aidha Dk. Never amesema katika kuongeza uzalishaji na ajira, kampuni hiyo imeanzisha kiwanda Moshi, mkoani Kilimanjaro na inaendelea kujenga kiwanda kingine Zanzibar.
Amesema kiwanda cha Moshi tayari kimewezesha ajira za moja kwa moja kwa vijana 20, huku ajira zisizo za moja kwa moja zikitokana na vijana na wazalishaji wanaosambaza bidhaa na vifaa mbalimbali vinavyotumika katika uzalishaji.
Pia Dk. Never amesema kampuni hiyo tayari imewawezesha wanawake 300, kupitia shughuli zinazohusiana na zao la mwani, Zanzibar na mkoani Tanga ambapo wengi wao ni vijana.
Amesema awali mwani ulikuwa ukikosa soko la kutosha kutokana na ukosefu wa viwanda vya ndani vya kuchakata na kuzalisha bidhaa mbalimbali zinazotokana na mwani, hali iliyowafanya wazalishaji kutegemea kuuza mwani ambao haujachakatwa nje ya nchi.
Amesema uwepo wa viwanda vya ndani unatoa fursa ya kutumia malighafi zinazozalishwa nchini na kuongeza thamani yake kabla ya kuuzwa katika masoko ya ndani na nje ya Tanzania.
“Lakini sasa kupitia Plant Biodefenders, inaonyesha kwamba Tanzania imewezekana,” amesema Dk. Never na kusisitiza viwanda vinaweza kuwa kichocheo cha kuwawezesha watu wengi zaidi wanaoshiriki katika uzalishaji.
Amesema bidhaa zinazozalishwa na kampuni hiyo zinatumiwa na kuuzwa katika mataifa mengine, bidhaa hizo zimefanyiwa utafiti na kuthibitishwa kufanya kazi kitaalamu na kuleta tija.
Mbali na uzalishaji, amesema Plant Biodefenders pia inatoa mafunzo kwa wakulima na vijana ili kuwajengea uwezo wa kibiashara na kuwaonyesha kuwa fursa za biashara zipo katika maeneo mbalimbali nchini.
Amesema katika mnyororo wa thamani wa kilimo, si lazima kila kijana awe mkulima, kwani anaweza kushiriki katika hatua nyingine kama kuuza mazao, kuwa wakala, kusambaza bidhaa au kuuza vifaa vya kufungashia mazao kama parachichi na bidhaa nyingine.
Ameeleza kuwa uelewa kuhusu mnyororo huo wa thamani umesaidia vijana kutambua kuwa wanaweza kupata kipato kupitia shughuli mbalimbali badala ya kutegemea ajira za Serikali au waajiri wengine.
Amesema changamoto kubwa iliyokuwepo ni ukosefu wa elimu na uelewa miongoni mwa vijana kuhusu fursa hizo, hivyo maonyesho ya Wiki ya Ubunifu Tanzania yamekuwa jukwaa muhimu la kuwafungua vijana na wanafunzi kuhusu namna ya kutumia fursa zilizopo nchini kujiajiri, kuanzisha biashara na hatimaye kujenga viwanda vinavyotengeneza ajira.


