Ulipaji Kodi wa Hiari ni Chachu ya Maendeleo ya Taifa-Mkurugenzi Kayombo


Dar Es Salaam

Mkurugenzi wa Idara ya Elimu kwa Mlipakodi na Mawasiliano wa Mamlaka ya Mapato Tanzania TRA, Richard Kayombo amesema kuwa ulipaji kodi wa hiari ndio msingi wa maendeleo kwa taifa letu na kila Mtanzania anawajibu wa kutimiza jukumu hilo ili kuiwezesha Serikali kutoa huduma bora.

Kayombo ametoa kauli hiyo Julai 3, alipokuwa akizungumza na Walipakodi waliotembelea Banda la TRA katika Maonyesho ya 50 ya kimataifa (Sabasaba) yanayoendelea ndani ya viwanja vya Sabasaba jijini Dar Es Salaam.

Amesema ushiriki wa TRA ndani ya Maonyesho ya Sabasaba unalenga kuwasogezea walipakodi huduma za kikodi karibu na kuwapatia elimu juu ya umuhimu wa ulipaji kodi wa hiari kama njia ya kuongeza kasi ya maendeleo nchini mwetu.

“Maendeleo tunayoyaona nchini kama ujenzi wa Barabara, Madaraja, Shule, Hospitali na miradi ya kimkakati yanatokana na kodi zinazolipwa na Wananchi. Hivyo ni muhimu kuendelea kuhamasika kulipa kodi kwa hiari ili kuisaidia serikali kuboresha maendeleo.” Alisema Kayombo.

Aidha, amewahimiza Wananchi kuendelea kuwa mabalozi wazuri wa kulinda na kutunza miundombinu ya umma, akieleza kuwa pale inapotokea uharibifu serikali hutumia kodi zetu kurekebisha badala ya kuzielekeza kutekeleza miradi mipya ya maendeleo.