Na MWANDISHI WETU, DAR ESSALAAM
MKUU wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, amesema waendesha bodaboda, Bajaj, Wamachinga na makundi ya Baba na Mama Lishe ni makundi muhimu yanachangia kukuza uchumi wa Tanzania, Serikali itaendelea kushirikiana nayo kuboresha mazingira ya kazi.
Mpogolo amesema hayo Mkoa Dar es Salaam wilayani Ilala katika mkutano uliwakutanisha Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Patrobas Katambi na makundi hayo ya Wamachinga, watoa huduma usafirishaji Bodaboda ,mama lishe na maguta.
"Hawa wamejiajili wenyewe, wanaendesha bodaboda zao bajaj,na biashara zao leo wameacha shughuli zao kwa muda ili kujadili amani na maendeleo ya nchi pamoja na viongozi wa Serikali "amesema Mpogolo .
Mpogolo amesema makundi yayo yamepata heshima ,fursa na mazingira bora ya kufanya kazi kutokana na falsafa ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan maridhiano,mageuzi,ujenzi mpya na utu.
Amesema miaka ya nyuma makundi hayo yalikuwa yakikumbana na changamoto nyingi, lakini sasa yanashirikishwa katika maamuzi na viongozi wakuu wa Serikali.
"Miaka 10 iliyopita hawa waliopo mbele yako walikuwa hawaruhusiwi kupita maeneo mbalimbali ya jiji, lakini leo wamekaa pamoja na Waziri wa Mambo ya Ndani, wamekutana na Rais na Waziri Mkuu. Hiyo ni heshima kubwa waliyopewa," amesema.
Amesema mafanikio hayo yametokana na maamuzi ya Rais Dk.Samia ya kujenga mazingira rafiki kwa wananchi wanaojiajiri ili waweze kufanya kazi kwa amani na kuchangia uchumi wa taifa.
Aidha, alisema falsafa ya Rais Dk. Samia inafanana na ile ya viongozi mbalimbali duniani wanaosisitiza kuwa maendeleo ya taifa huanza kwa kuwajali wananchi.
Mpogolo amesema Serikali imeendelea kutenga fedha kwa ajili ya mikopo kupitia halmashauri pamoja na kujenga masoko ili kuboresha mazingira ya wafanyabiashara wadogo.
Pia aliomba kuimarishwa kwa ushirikiano kati ya Jeshi la Polisi, LATRA na viongozi wa bodaboda ili kuongeza elimu ya usalama barabarani na kuhakikisha sheria zinafuatwa.


