Na Mwandishi wetu, Sumbawanga
Wadau wa maendeleo ndani na nje ya Mkoa wa Rukwa, wamehamasishwa kuchangia upatikanaji wa madawati ili watoto wasome katika mazingira wezeshi kwa ustawi wa taaluma.
Wito huo umetolewa hivi karibuni na Mbunge wa Jimbo la Kwela, ambaye pia ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, Deus Sangu, alipokabidhi madawati kwa shule za msingi katika jimbo hilo alipofanya ziara ya kikazi.
Sangu amekabidhi madawati zaidi ya 100 kwa shule za msingi sita, yenye thamani ya Shilingi milioni 60, ameyapata kupitia ufadhili ya Benki ya Taifa ya Biashara (NBC).
Waziri Sangu akizungumza kwenye moja ya mikutano yake na wananchi wa kijiji cha Nankanga tarafa ya Kipeta na kijiji cha Ilemba alisema ametoa msaada huo kuunga mkono jitihanda za wananchi katika kuchangia maendeleo ya elimu.
“ Nimekuja hapa kukabidhi zawadi ndogo kwa watoto. Leo nimewaletea madawati 20 yatasaidia watoto 60 kutoendelea kukaa chini” amesema Waziri Sangu.
Mbunge huyo aliongeza kuwaambia wananchi kuwa yeye ni mbunge wa vitendo na kwamba anapenda vitu vinavyoonekana ambapo aliitumia fursa hiyo kushukuru uongozi wa Benki ya NBC kwa kuguswa na shida za wanaKwela .
“Ninashukuru benki ya NBC kwa msaada wao waliotupatia madawati haya yanayokwenda kupunguza tatizo la watoto kukaa chini. utatuzi huu wa kero za wananchi ni sehemu ya maelekezo tuliyopewa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwetu wabunge” alisema Sangu alipoongea na wananchi wa Kijiji cha Msia kata ya Milepa huku akitoa wito kwa wadau wengine wa maendeleo kuchangia madawati kwa ajili ya jimbo la Kwela.
Miongoni mwa shule zilizopokea madawati hayo na idadi yake kwenye mabano ni shule ya msingi Kalumbaleza (20), Msia (20), Kimambo (15), Ilemba (20) , Nankanga (20) na Deusi Sangu sekondari madawati (30).
Akizungumza kwa niaba ya wananchi, Diwani wa Kata ya Mwadui, Mahmood Mgweno, amesema amepokea madawati kutoka Ofisi ya mbunge na tayari amefikisha shuleni na kumpongeza Mbunge Sangu kwa msaada.
Kwa upande wa wananchi wametumia fursa ya ziara ya mbunge Sangu kueleza kufurahishwa kwao na jitihada anazozifanya kuchangia maendeleo ya jimbo hilo ikiwemo msaada wa madawati.
Naye Thomas Nsandale ameishukuru Ofisi ya Mbunge kwa kuwezesha wa upatikanaji wa madawati ikiwa ni miongoni mwa vingi walivyopatiwa katika kipindi chote Sangu akiwa Mbunge wa Jimbo la Kwela.
“Sangu amefanya mambo mengi ambayo yanatufanya sisi wananchi kutokupunguza upendo juu yake na tunamuomba pia Madawati haya yasiwe ya mwisho kwa wananchi wake wa Kwela Bali iwe sababu ya muendelezo wa Maendeleo haya” amesema Nsandale.
Waziri Sangu alikuwa jimboni Kwela wilaya ya Sumbawanga kukagua shughuli za maendeleo pamoja na kuzungumza na wananchi.

