TANOIL Yawaita Wadau wa Mafuta ya Dizeli na Petroli kwa Uhakika wa Mafuta


KAMPUNI tanzu ya Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), TANOIL imetoa wito kwa wadau wa masuala ya mafuta ya petroli na dizeli kujiunga na kampuni hiyo kwa uhakika zaidi wa mafuta nchini.

Tanoil imeelezea dhamira yake ya kuendelea kupanua wigo wa biashara zake kwa kuanza uuzaji wa gesi ya petroli iliyoshindiliwa kwenye mitungi (LPG), sambamba na shughuli zake za usambazaji wa mafuta ya petroli na dizeli.

Akizungumza katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba), Julai 3, 2026 Afisa Masoko wa TANOIL, Grace Chigugu, amesema kampuni hiyo ilianzishwa mwaka 1999 na kuanza kutekeleza majukumu yake kama kampuni ya masoko ya mafuta (Oil Marketing Company - OMC) mwaka 2021.

Alisema TAN OIL imepewa jukumu la kufanya biashara ya uuzaji wa mafuta ya petroli na dizeli kwa jumla, huku ikiendelea kuimarisha huduma zake kwa wateja mbalimbali nchini.

Chigugu alisema katika mpango wa kupanua shughuli za biashara, kampuni hiyo inatarajia kuanza biashara ya gesi ya petroli iliyoshindiliwa kwenye mitungi ili kuwafikia Watanzania wengi zaidi.

Aidha, alisema TAN OIL inamiliki vituo vya mafuta katika maeneo mbalimbali nchini, ikiwemo Geita, Singida, Musoma na Tarime, hatua inayowezesha huduma zake kuwafikia wateja kwa ufanisi.

Aliwataka wamiliki wa vituo vya mafuta, viwanda, migodi na wakandarasi kushirikiana na TAN OIL, akieleza kuwa kampuni hiyo ya serikali ni mshirika wa kuaminika anayezingatia maendeleo ya taifa pamoja na mafanikio ya wateja wake.

Alibainisha kuwa TAN OIL kwa sasa inahudumia wateja mbalimbali, wakiwemo taasisi za serikali, migodi, vituo vya mafuta na wakandarasi, huku akisema mwitikio wa huduma zao unaendelea kuongezeka.

"Tunatoa rai kwa wadau wote kufanya kazi na TAN OIL kwa kuwa watapata uhakika wa upatikanaji wa mafuta, huduma bora kwa wateja na ushirikiano unaozingatia ubora, uaminifu na ubunifu," alisema Chigugu.

Aliongeza kuwa kwa kuwa TAN OIL ni kampuni ya serikali, wateja wana uhakika wa kupata mafuta kwa wakati na kwa utaratibu unaoaminika bila usumbufu.