Meya Sheta afungua ofisi ya Diwani Kata ya Kisutu



Na MWANDISHI WETU

Meya wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Nurdin Bilal ‘Sheta’ amefungua rasmi Ofisi ya Diwani Kata ya Kisutu, Tousif Mohammedali Bhojani na  kumtaka diwani  huyo kukaa ofisini kusikiliza na kutatua kero za wananchi badala ya kumweka mwakilishi.


Sheta alifungua ofosi hiyo leo  baada ya ukarabati mkubwa uliofanywa na Diwani Bhojani wenye lengo la  kuandaa mazingira bora ya kuwahudumia wananchi.


“Usiweke mwakilishi wa kusikiliza kero  za  wananchi. Kaa wewe ofisini uwasikilize. Rais Dk. Samia Suluhu Hassan anatutaka  tusikilize na kutatua kero za wananchi wetu. Huu ni utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM). Wananchi wa Kata ya Kisutu njooni katika ofisi yenu hii na kero zenu  zitatatuliwa na zikishindikana leteni katika ofisi yangu,”amesema Sheta.


Kwa upande wa Diwani Bhojani amesema lengo la kukarabati ofisi hiyo ni kutekeleza  ahadi  aliyoitoa ya kuifanya  kuijenga Kisutu Mpya, inayo tatua na kusikiliza kero za wananchi.


“Katika ofisi hii  nitakuwepo Jumatano na Alhamisi kusikiliza  na kutatua kero za wananchi.  Wananchi wa Kisutu walikuwa na shida kwa sababu hawakujua ni wapi wanapeleka shida zao  ngazi ya  kata. Sasa ofisi ipo na tumeiboresha. Waje tutawahudumia vizuri,” ameeleza Bhojani.


Naye Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Ilala, Said Sidde, alipongeza hatua ya diwani huyo kukarabati ofisi hiyo  na kuwataka wananchi kuitumia   kwani Chama kimetoa maelekezo kwa madiwani , watendaji na watumishi wa serikali kuhakikisha wanawasikiliza wananchi na kutafuta ufumbuzi wa changamoto zao.


Baadhi ya wananchi wa kata hiyo  wamesema  nuru njema imeanza  kuonekana  tangu diwani huyo aingie madarakani kwani amekuwa karibu na wananchi  hivyo imekuwa ni rahisi  kusikilizwa kero zao. 



Meya Sheta afungua ofisi ya Diwani Kata ya Kisutu Meya Sheta afungua ofisi ya Diwani Kata ya Kisutu Reviewed by Gude Media on January 16, 2026 Rating: 5

Boxed Width - True/False

True