FCC Yawafungulia Milango Wafanyabiashara na Wajasiriamali Geita, Yatoa Elimu ya Ushindani


Na MWANDISHI WETU

TUME ya Ushindani (FCC) kwa kushirikiana na Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara (TanTrade), imetoa mafunzo kwa wafanyabishara na wajasiriamali wa Wilaya ya Geita ambao wanashiriki katika Maonesho ya Tisa ya Kitaifa ya Teknolojia ya Madini wakuze biashara zao.

‎Mafunzo hayo yametolewa Oktoba Mosi, 2026 ni sehemu ya Kliniki ya Biashara iliyo chini ya Mwamvuli wa TanTrade ambapo Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Viwanda na Biashara ikiwemo FCC zinashiriki kutoa huduma kwa wananchi katika maonesho hayo yanayoendelea katika Viwanja vya Dk. Samia Suluhu Hassan mkoani Geita. 

‎Akizungumza na wajasiriamali katika banda la Wilaya ya Geita, Ofisa Uhusiano wa Umma Mkuu wa FCC, Nsajigwa Wilfred, amesema lengo kubwa la kushiriki katika maonesho hayo ni kutoa huduma kwa wafanyabishara na wajasiriamali, wafahamu majukumu ya msingi ya Tume hiyo katika kulinda na kushajiisha ushindani wa biashara.

Pia, amesema ni kudhibiti bidhaa bandia, kumlinda mlaji ikiwa ni pamoja na kupokea maoni au ushauri wa kitaalam kuhusu changamoto zinazowakabili na kuona namna bora ya kuzitafutia majawabu muafaka kwa wakati sahihi. 

‎Aidha, Nsajigwa amebainisha kuwa FCC ina jukumu la msingi katika kusimamia na kutekeleza Sheria ya Ushindani Namba 8 ya Mwaka 2003 (FCA) ambayo ina jukumu la kulinda na kushajiisha ushindani wa biashara ili kuhakikisha ushindani wa biashara unafanyika kwa haki na kwa kuzingatia misingi madhubuti ya sheria, kanuni na taratibu katika nyanja ya uchumi wa soko.

‎Kwa upande wa Meneja Ukuzaji Biashara wa TanTrade, Deo Shayo, amewaasa wafanyabiashara na wajasiriamali hao kusajili bidhaa zao kwa chapa ya 'Made in Tanzania' ili ziweze kutambulika kimataifa na kuipa nguvu chapa ya Tanzania,  kuimarisha uchumi na kuchochea uwekezaji na uzalishaji.

‎"Mjisikie fahari kuuza bidhaa zenu zikiwa na chapa ya Made in Tanzania ili kuipa nguvu chapa ya Tanzania, kuimarisha uchumi na kuchochea uwekezaji na uzalishaji, " amesema Shayo.