Watu Wanne Wafariki Ajali ya Basi na IST Bunju


Na MWANDISHI WETU

WATU wanne wamefariki dunia baada ya basi la Kampuni ya Abood kugongana na gari ndogo aina ya Toyota IST katika eneo la Bunju Sokoni, Dar es Salaam.

Ajali hiyo ilitokea Septemba 7, 2026, saa 7:40 usiku katika barabara ya Bagamoyo, wakati basi lenye namba za usajili T 235 EMJ, aina ya Yutong, likitokea Tegeta kuelekea Bunju kwa safari ya kwenda mkoani Tanga.

Kwa mujibu wa taarifa ya Jeshi la Polisi, waliopoteza maisha katika ajali hiyo ni Hamad Mohamed Juma maarufu Majid, Edward Kimanyara, mstaafu na mkazi wa Yombo Dovya, Temeke, Magdalena Manyenga, mkazi wa Temeke na Melina Emmanuel Kayoka, mkazi wa Yombo Kisiwani, Temeke.

Basi hilo lilikuwa likiendeshwa na Christivian Shemuhilu, mkazi wa Kange, Tanga.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa basi hilo liligongana na gari lenye namba T 274 ERU, aina ya Toyota IST, lililokuwa likiendeshwa na Majid, mkazi wa Mtoni Mtongani.

Chanzo cha ajali ni uzembe wa dereva wa basi, ambaye alifanya kitendo cha kuyapita magari mengine (Overtake), bila kuchukua tahadhari dhidi ya watumiaji wengine wa barabara.

Miili ya marehemu imehifadhiwa katika Hospitali ya Mwananyamala, Kinondoni, Dar es Salaam.

Dereva wa basi hilo, Christivian Shemuhilu, anashikiliwa kwa ajili ya hatua zaidi za kisheria.

Jeshi la Polisi limetoa wito kwa watumiaji wote wa barabara, hususan waendesha vyombo vya moto, kuendelea kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za usalama barabarani ili kuzuia na kuepusha ajali.