Ashikiliwa kwa Tuhuma za Kumshambulia Askari wa Usalama Barabarani


Na MWANDISHI WETU

POLISI Kanda Maalumu ya Dar es Salaam inamshikilia mkazi wa Lugalo na Mloganzila, Conrad  Kayoza, kwa tuhuma za kumshambulia kwa ngumi na mateke askari wa Usalama Barabarani aliyekuwa akitekeleza majukumu yake.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro, tukio hilo limetokea Septemba 8, 2026, saa 1:30 asubuhi katika eneo la Lugalo, Kinondoni, Barabara ya Bagamoyo.

Taarifa hiyo inaeleza askari Polisi namba F. 8886 SGT Andrew, kutoka Kikosi cha Usalama Barabarani Kinondoni, alikuwa akitekeleza majukumu yake kwa kuyazuia kisheria magari yaliyokuwa yakipita pembezoni mwa barabara, maarufu 'Service Road', nje ya utaratibu.

Miongoni mwa magari yaliyokuwa yamezuiwa ni gari lenye namba za usajili T 455 EER, aina ya Toyota Runx, linalodaiwa kuwa la mtuhumiwa huyo.

Kwa mujibu wa Polisi, baada ya gari hilo kuzuiwa, Kayoza alishuka na kuanza kumshambulia askari huyo kwa ngumi na mateke.

Hata hivyo, tukio hilo liliwafanya wananchi waliokuwa eneo hilo kuchukizwa na kitendo hicho na kumshambulia mtuhumiwa.

Polisi imesema Kayoza amepelekwa hospitalini kwa matibabu na  baada ya kupata nafuu atahojiwa kwa kina ili hatua za kisheria zichukuliwe na mamlaka husika.

Katika taarifa hiyo, Polisi imetoa tahadhari na onyo kali kwamba haitavumilia wala kusita kuchukua hatua kali za kisheria na za haraka dhidi ya mtu yeyote au kundi litakalowashambulia askari Polisi wanapotekeleza majukumu yao ya kisheria.