Royal Queens Zanzibar Wajiwindaa kwa Mapinduzi Cup


NA MWANDISHI WETU

TIMU ya wanawake ya mchezo wa Hockey  ya Royal Queens kutoka Zanzibar, imeanza kujiandaa na michuano  ya Mapinduzi Cup  inayotarajiwa kufanyika mapema mwakani  ambapo imefanya mazoezi ya pamoja  na wachezaji wa mchezo hao Tanzania Bara.

Akizungumza na gazeti hili jijini Dar es Salaam,  Mwenyekiti wa Chama cha Hockey Zanzibar , Juma Hassan Juma, amesema ni kwa mara ya kwanza  timu ya Hockey  ya wanawake kutoka Zanzibar  kutua jijini  humo kufanya mazoezi ya pamoja na wachezaji wa mchezo huo Tanzania bara.

Amesema ,  mazoezi hayo ya wiki moja yamekuwa na ufanisi mkubwa  katika kuwanoa  wachezaji wa timu hiyo ya wanawake.

"Tunaahidi  kufanya vizuri  katika michuano ya Mapinduzi Cup inayotarajiwa kufanyika Januari mwakani,"amesema Juma.

Ameeleza, changamoto iliyokuwepo awali Zanzibar ni kukosekana kwa viwanja maalumu vya mchezo huo  ingawa 

kuna mwamko wa jamii kushiriki na kuupenda mchezo huo huku akiishukuru Serikali chini ya Rais  wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi, kuanza ujenzi wa viwanja mbalimbali na hamasa kubwa ya kuinua sekta ya michezo.

Ametoa wito kwa jamii na wahisani   kusaidia  kukuza mchezo huo  wa Hockey  hususan timu za majeshi  Zanzibar kutoa wachezaji ambao watashiriki katika timu za wanawake za mchezo huo. 

Kipa  timu hiyo ya Royal  Queens, Idaya Hassan,  amesema  mazoezi hayo ya pamoja yaliyofanyika katika viwanja vya JMK Youth Park, jijini Dar es Salaam, yamekuwa na  ufanisi  na yamesaidia wachezaji wa timu yake  kujinoa kikamilifu.

Mratibu wa mchezo wa Hockey  katika shule za  Tanzania Bara , Elieza Mwankemwa, amesema  mazoezi hayo ya wiki moja 

yameambatana na  mafunzo mbalimbali kuiimnarisha timu hiyo ya  wanawake  kwani Zanzibar ilikuwa na  timu nyingi za wanaume.