Diwani Selemani Kaniki Azindua Kampeni ya Kuwapatia Wananchi Hati za Ardhi


Na Mwandishi Wetu

DIWANI wa Kata ya Zingiziwa, Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Selemani Kaniki (CCM), amezindua kampeni ya kuwapatia wananchi wa kata hiyo hati miliki za ardhi, ikiwa ni kuwawezesha kupata utambuzi na ulinzi wa kisheria wa maeneo yao.

Akizungumza katika uzinduzi wa kampeni hiyo, Kaniki amesema kampeni hiyo itakuwa endelevu na itahusisha utoaji na ugawaji wa hati za ardhi kwa wakazi wa kata hiyo, Wilaya ya Ilala.

“Nimezindua zoezi hili leo kwa sababu ni hatua muhimu katika kuhakikisha wananchi wanapata utambuzi na ulinzi wa kisheria wa ardhi na kuongeza usalama wa mali zao na uwekezaji wa familia,” amesema Kaniki.

Amesema wananchi wa kata hiyo wataendelea kuhamasishwa kushiriki kikamilifu na kutumia fursa hiyo muhimu ya kupata hati za ardhi.

Kaniki amesema mafanikio ya kampeni hiyo itaendelea kupatikana kupitia juhudi za ufuatiliaji na usimamizi, kuhakikisha huduma hiyo inawafikia wananchi wengi zaidi.

Pia Kaniki amewataka wananchi kuunga mkono juhudi za Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, akisema serikali imeleta miradi mikubwa ya maendeleo katika Kata ya Zingiziwa, ikiwemo katika sekta za afya, elimu na miundombinu ya barabara.