Barrick Bulyanhulu Yafanikisha Ujenzi wa Kituo cha Polisi Nyang'hwale - GUDE MEDIA

Breaking

9/28/26

Barrick Bulyanhulu Yafanikisha Ujenzi wa Kituo cha Polisi Nyang'hwale

 


Na MWANDISHI WETU

Katika mwendelezo wa kuunga mkono jitihada za Serikali za kuleta maendeleo na kulinda usalama wa raia, Mgodi wa Barrick Bulyanhulu, kupitia Fedha za Uwajibikaji kwa Jamii (CSR), umefanikisha ujenzi wa Kituo kidogo cha Polisi katika stendi ya mabasi ya Ikangala, wilayani Nyang'hwale mkoani Geita.

Akizungumza katika hafla ya kukabidhi kituo hicho, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Nyang’hwale Ntiriyo Ezekiel, amesema kituo hicho kinajumuisha sehemu ya mahabusu na ofisi ya Meneja wa kituo na tayari kimekamilika kwa asilimia 100.

“Halmashauri ilipokea fedha za CSR shilingi milioni 36.6 kutoka Barrick Bulyanhulu ambapo kwa kushirikiana na ofisi Kamanda wa Polisi wa wilaya ilianza utekelezaji wa ujenzi”, amesema.

Ezekiel amesema Barrick Bulyanhulu pia imefanikisha ujenzi wa stendi ya mabasi ya kisasa ya Ikangala, ambapo uwepo wa kituo hicho utaimarisha ulinzi na usalama wa abiria na mali zao, ikiwemo kuwahudumia wananchi wanaoishi maeneo ya jirani na kituo hicho.

Kwa upande wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Safia  Jongo, ametoa shukrani kwa Kampuni ya Barrick kwa kuwa mstari wa mbele kuunga mkono jitihada za serikali katika kuimarisha usalama wa raia.

Amesema kituo hicho kitasaidia kuimarisha ulinzi katika kituo hicho cha mabasi na kuwa msaada kwa abiria, wamiliki wa vyombo vya usafiri na kuwezesha askari polisi kufanya kazi ya kuwahudumia wananchi katika mazingira rafiki.

Safia amesema Polisi Mkoa wa Geita litaweka Dawati la masuala ya kijinsia  na ustawi wa jamii, kushugulikia kesi za  unyanyasaji wowote wa kijinsia.

Pia amemtaka Mkurugenzi wa halmshauri hiyo kuweka utaratibu mzuri kwa mawakala na wapiga debe ndani ya stendi kwa kuwapa sare na vitambulisho, kuepuka abiria kuibiwa mali zao wakiwa ndani ya stendi.

Mwakilishi wa mgodi wa Barrick Bulyanhulu, William Chungu ambaye ni Afisa Mahusiano ya Jamii, amesema  Barrick kupitia migodi yake nchini  itaendelea kushirikiana na Serikali katika masuala mbalimbali ikiwemo kutekeleza miradi ya kimkakati ambayo itanufaisha wananchi  hususani wanaoishi maeneo ya jirani.

Chungu aliongeza kuwa kukamilika kwa mradi huu ni hatua muhimu katika kuboresha huduma za usafiri, kuimarisha usalama wa abiria na mali zao pamoja na kuweka mazingira bora kwa shughuli za kiuchumi katika eneo la stendi.

Ameongeza kuwa kukamilika kwa mradi huu ni hatua muhimu katika kuboresha Huduma za usafiri, kuimarisha usalama wa abiria na mali zao pamoja na kuweka mazingira bora kwa shughuli za kiuchumi katika eneo la stendi.

Barrick ambayo inaendesha shughuli zake nchini kwa ubia na serikali kupitia kampuni ya Twiga imekuwa ikishirikiana na serikali kupitia jeshi la polisi kufanikisha usalama kwa raia ambapo mwaka juzi  ilikabidhi msaada wa vifaa vya kisasa vya kupima ulevi vyenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 100 za Kitanzania kwa Jeshi la Polisi Kitengo cha Usalama Barabarani ikiwa ni mwendelezo wa kampeni ya Barrick ya ‘Journey to zero’ ambayo inalenga kuhamasisha afya na usalama kwa wafanyakazi wake na wadau wengine wote kwenye jamii.

Pia Barrick imekuwa mstari wa mbele kushirikiana na wadau mbalimbali wanaotoa elimu ya ukiukaji wa haki za Binadamu ikiwemo ukatili wa kijinsia ambapo imekuwa ikishirikiana  na Jeshi la Polisi kufikisha elimu ya kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsia kwenye jamii.




No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.