Na MWANDISHI WETU
Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar ameweka jiwe la msingi kwenye ujenzi wa Ofisi za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Zinazotarajiwa kujengwa Kizimkazi Visiwani Zanzibar lengo likiwa ni kusogeza karibu na Wananchi huduma za Kodi.
Akiweka jiwe hilo la msingi Agosti 13, 2026 Balozi Khamis Mussa Omar amesema kupitia ofisi hiyo itakayowahudumia wananchi wa Kizimkazi na Paje pamoja na ofisi nyingine za TRA zilizopo nchi nzima huduma za kodi zitaboreka zaidi na kuwapunguzia wananchi kadhia ya kufuata huduma mbali na maeneo yao.
Balozi Omar amesema maendeleo makubwa yanayoonekana nchini yanatokana na Kodi za wananchi na kuipongeza TRA kwa juhudi inazofanya katika kukusanya kodi za wananchi na kuvuka malengo wanayopangiwa na Serikali ambapo kwa mwezi Julai pekee kwa mwaka wa fedha 2026/2027 walitakiwa kukusanya Sh. Trilioni 2.971 lakini imekusanya Sh. Trilioni 3.245 sawa na asilimia 109 na ukuaji asilimia 21.
Amesema kukusanya kodi ni mzunguko wa ukuaji wa uchumi wa nchi na mwananchi mmoja mmoja na kuwataka watanzania waone fahari kulipa kodi kwani watakuwa wamechangia katika maendeleo ya Taifa.
Kwa upande wake Kamishna Mkuu wa TRA, Yusuph Juma Mwenda amesema Mamlaka hiyo imeweka mkakati wa kuendelea kusogeza karibu zaidi huduma na wananchi kwa kujenga ofisi nyingi na kwa mwaka wa fedha wanatarajia kujenga jumla ya ofisi 49 kwa nchi nzima.
Amesema lengo la kusogeza huduma karibu na wananchi ni kutaka kuokoa muda wa wananchi kufanya shughuli zao za kiuchumi.
Amesema TRA itaendelea kutoa huduma bora kwa wananchi wote bila kumpendelea wala kumuonea mtu huku akiweka wazi kuwa wataendelea kupambana na wote wanaokwepa kodi na kutoa rai kwa wananchi kuwafichua.
Katika hatua nyingine Kamishna Mkuu Mwenda ametembelea banda la TRA lililopo kwenye Kizimkazi Festival kwaajili ya kutoa huduma kukabidhi Vyeti vya namba za utambulisho wa Mlipakodi (TIN) kwa baadhi ya wananchi waliotembelea banda hilo akisisitiza kuwa Wafanyabiashara wanaopatiwa TIN mpya watakapa msamaha wa kodi kwa muda wa mwaka mmoja.
Amesema utaratibu huo unalenga kusajili walipakodi wengi zaidi ili kuongeza wigo wa kodi na kukuza biashara nchini hali ambayo itasaidia kuchochea shughuli za uchumi kwa wananchi.
Mwenda amesema katika utendaji kazi wake TRA imekuwa ikiwafuata wananchi katika maeneo yao ya biashara kuwasikiliza, kutatua changamoto zao na kuwezesha biashara zao.
Kamishna Mkuu Mwenda ametoa wito kwa Walipakodi kutembelea maonyesho ya biashara kwenye Kizimkazi Festival ili kupata huduma za TRA zinazoendelea kutolewa.
Kwa upande wake mmoja wa wananchi waliopatiwa TIN, Yusuph Mabrook Juma ameishukuru TRA kwa kuwasogezea huduma karibu na maeneo yao na kuwapatia elimu ya kodi itakayowawezesha kutambua umuhimu wa kulipa kodi.
Amesema katika banda la TRA pia amepatiwa elimu ya namna ya kuendesha biashara zake hali ambayo itamsaidia kuinuka kiuchumi.

.jpeg)