Na MWANDISHI WETU
SPIKA WA Bunge ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Ilala, Mussa Zungu, amewataka Wanawake kushirikiana na kupendana kuwa wamoja na wasiwe na wivu wa mafanikio ya wezao.
Zungu, amesema hayo katika Kongamano la Wanawake (Bonyokwa Women Gala), lililoandaliwa na Diwani wa Kata ya Bonyokwa, Tumike Malilo, limewashirikisha Wanawake wote wa Wilaya ya Ilala, mkoani Dar es salaam.
"Natumia fursa hii kumpongeza mwanamke mwezenu wa Kata ya Bonyokwa, Tumike Malilo, kwa kuandaa jambo kubwa hili la kuwakutanisha Wanawake wote wa Ilala katika Bonyokwa Women Gala nawaomba Wanawake mshirikiane mpendane muwe wamoja mtafanikiwa, "amesema Zungu.
Pia Zungu amewapongeza wanawake kwa kupata elimu ya ujasiriamali kutoka kwa wadau mbalimbali wakiwemo taasisi za fedha ,DAWASA, SIDO, Halmashauri ambapo aliwataka wanawake hao elimu hiyo waliopata waende kuitumia katika kukuza uchumi waweze kumsaidia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan katika kujenga Tanzania ya uchumi na viwanda.
Zungu amewataka wanawake kuwa na nidhamu na kujitafutia uchumi, ikiwemo kuunda viwanda vidogo na kukopa biashara ya Bodaboda zikawa maalumu kwa kusafirisha mizigo mbalimbali ambayo itawaingizia kipato.
Akizungumzia mikopo ya Serikali ya asilimia kumi ambayo inatolewa ngazi ya Halmashauri, Zungu alisema Taasisi za fedha wameweka vigezo vikubwa kupelekea wananchi kushindwa kukopa mikopo hiyo mpaka sasa hivi Ilala kuna shilingi bilioni 17.
Kwa upande mwingine aliwataka wanawake hao wawe kifua mbele mashindano ya AFCON yatakapoanza wachangamkie fursa kwa ajili ya kukuza uchumi kwani kutakuwa na kazi nyingi za uzalishaji uchumi.
Diwani wa Kata ya Bonyokwa Tumike Malilo, alisema dhumuni maalum la siku hiyo kumpongeza Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan, kwa kufanya mambo makubwa kata ya Bonyokwa sekta ya Elimu, sekta ya Afya,miundombinu ya Barabara, sasa hivi Bonyokwa inaenda kuwa ya kisasa.
Mwenyekiti Umoja wanawake UWT mkoa Dar es Salaam Mwajabu Mwambo ,alitumia fursa hiyo kumpongeza Diwani Tumike Malilo,kwa kuunga mkono juhudi za Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan,
Mwajabu Mwambo alitumia fursa hiyo pia kuwaasa wanawake wa Wilaya ya Ilala akisema Wanawake wana Jukumu kubwa katika malezi ya familia hivyo aliwataka Wazazi kuwalea watoto katika malezi bora sambamba na kupata elimu.
"Wazazi ni walezi wa familia nawaomba Wazazi wezangu tuangalie watoto wetu katika vitendo vya ukatilia wa kijinsia tutenge wakati kuwa nao pamoja na kuwakagua"alisema Mwajabu.


