DED Igunga Awaongoza Watumishi na Wananchi Kufanya Usafi wa Mazingira


IGUNGA, TABORA

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Igunga mkoani Tabora, Selwa Hamid, amewaongoza watumishi na wananchi kufanya usafi wa mazingira katika eneo la Sabasaba, mjini Igunga, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuendelea kuuweka mji huo katika hali ya usafi muda wote.

Zoezi hilo limefanyika baada ya Mkurugenzi huyo kushiriki jogging, ambapo alihitimisha shughuli hiyo kwa kuwaongoza watumishi na wananchi katika kufanya usafi wa mazingira katika eneo hilo.

Akizungumza wakati wa zoezi hilo, Selwa amewakumbusha wananchi kujitokeza kwa wingi kushiriki katika mapokezi na shughuli mbalimbali za Mbio za Mwenge wa Uhuru, unaotarajiwa kukimbizwa katika Wilaya ya Igunga ifikapo Septemba 20, 2026.

Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Usafi wa Mazingira wa Halmashauri hiyo, Joseph Mafuru, amewashukuru wadau mbalimbali, wakiwemo Jeshi la Polisi, kwa kujitolea na kushiriki kikamilifu katika zoezi hilo la usafi.

Amesisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya wananchi na taasisi mbalimbali katika kuhakikisha mazingira ya mji wa Igunga yanakuwa safi na salama wakati wote.