Na Heri Shaaban (Ilala)
Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, amewataka wafanyabiashara wote wilayani humo kushiriki kikamilifu kampeni ya Serikali ya usafi, kupendezesha Jiji la Dar es Salaam na kulifanya liwe na mazingira safi na ya kuvutia.
Mpogolo ametoa wito huo, Julai 25, 2026, Dar es Salaam, katika kampeni endelevu ya usafi wa mwisho wa mwezi iliyowashirikisha watumishi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilala, kampuni za usafi zikiwemo SATEK na JUZA na wananchi.
"Natoa agizo kwa wafanyabiashara wote waliopo Wilaya ya Ilala kushirikiana na Serikali katika kuhamasisha kampeni hii ya usafi kwenye maeneo yao ya biashara wakati wote, hususan kila Jumamosi. Vilevile, kampuni zote za usafi na wakandarasi wa ukusanyaji taka wahakikishe wanatimiza wajibu wao wa kuondoa taka kwa wakati ili kuepusha mrundikano wa taka mbele ya maduka na maeneo ya biashara," amesema Mpogolo.
Aidha, alitumia fursa hiyo kuwapongeza madiwani wa Ilala, wenyeviti wa serikali za mitaa, wakandarasi wa ukusanyaji taka wa kampuni za SATEK na JUZA na wananchi kwa ushirikiano wao uliofanikisha zoezi hilo la usafi.
Mpogolo amesema kampeni hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ya kuboresha huduma za afya kupitia ujenzi na uimarishaji wa vituo vya afya, zahanati na hospitali nchini.
Amesema uwekezaji mkubwa unaofanywa na Serikali katika sekta ya afya hautakuwa na tija ikiwa wananchi hawatazingatia usafi wa mazingira wanayoishi na kufanyia shughuli zao za kila siku.
"Afya bora huanzia kwenye kinga, na usafi ni nguzo muhimu katika kujikinga dhidi ya magonjwa. Nawashukuru wenyeviti wa serikali za mitaa kwa kujitolea kwenu katika kuhamasisha usafi. Naiomba Ilala nzima iendelee kuwa safi kwa kuendeleza kampeni hii ya Serikali ya kufanya usafi kila siku, pamoja na kushiriki kikamilifu zoezi la usafi wa mwisho wa mwezi kwa kushirikiana na wananchi," amesema Mpogolo.


