DC Mpogolo Apiga Marufuku Madanguro Ilala


Na MWANDISHI WETU

Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, ametangaza msako mkali dhidi ya madanguro na vitendo vya ukiukwaji wa maadili, akisisitiza kuwa Serikali haitamvumilia mtu yeyote anayejihusisha na biashara hizo au kuwatumia watoto katika vitendo vya unyanyasaji.

Mpogolo ametoa kauli hiyo jijini Dar es Salaam, alipokuwa akizungumza na wananchi wa Kata ya Zingiziwa katika kikao cha kusikiliza na kutatua kero za wananchi.

"Natangaza msako mkali dhidi ya madanguro na vitendo vya ukiukwaji wa maadili. Serikali haitamvumilia mtu yeyote anayefanya biashara hizo au anayewatumia watoto katika vitendo vya unyanyasaji," amesema Mpogolo.

Amesema taarifa zilizopo zinaonesha kuwa katika Kata ya Zingiziwa, kulikuwa na mtu anayeshukiwa kuwatumia watoto wa kike kuwachezesha wakiwa uchi kwa malipo ya kati ya shilingi 3,000 na 5,000, jambo alilolieleza kuwa ni ukatili mkubwa na ukiukwaji wa maadili ya jamii.

Mpogolo amesema mtuhumiwa huyo tayari amekamatwa na Jeshi la Polisi na kwamba uchunguzi unaendelea. Alifafanua kuwa mara baada ya upelelezi kukamilika, mtuhumiwa atafikishwa katika vyombo vya sheria ili hatua stahiki zichukuliwe.

Aidha, amempongeza Kamanda wa Polisi wa Wilaya na askari wote waliohusika kwa kuchukua hatua mapema kabla madhara hayajaongezeka.

Mkuu huyo wa Wilaya amewataka wenyeviti wa mitaa na wananchi kushirikiana kwa karibu na vyombo vya dola ili kuhakikisha madanguro yanatokomezwa. Alisisitiza kuwa hakuna nafasi ya biashara zinazoharibu maadili ya jamii na kuhatarisha usalama wa watoto pamoja na familia.

Mpogolo amesema umaskini hauwezi kuwa kisingizio cha kuwahusisha watoto au wanawake katika vitendo vinavyodhalilisha utu wa binadamu. Alionya kuwa jamii ikiendelea kuvifumbia macho vitendo hivyo, itakuwa inahatarisha mustakabali wa kizazi kijacho.

Pia amewahimiza viongozi wa dini na jamii kuendelea kusimamia maadili mema, akisema haiwezekani kupinga maovu makanisani na misikitini huku yakiachwa yaendelee katika maeneo ya makazi.

Wakati huo huo, ameipongeza Ofisi ya Kamanda wa Polisi wa Mkoa (RPC) pamoja na Mkuu wa Polisi wa Wilaya (OCD) kwa operesheni zilizofanyika hivi karibuni, akieleza kuwa zaidi ya watu 20 walikamatwa katika msako dhidi ya vitendo hivyo.

Amesema operesheni hizo ni sehemu ya jitihada za Serikali za kurejesha maadili, kulinda watoto na kuimarisha usalama wa wananchi katika Wilaya ya Ilala.