Takwimu Sahihi Zatajwa Msingi wa Maendeleo ya Taifa


Na MWANDISHI WETU

NAIBU Waziri wa Fedha, Mshamu Munde, amesema takwimu sahihi ni msingi muhimu katika kupanga na kutekeleza mipango ya maendeleo ya taifa, akisisitiza kuwa mafanikio ya sekta mbalimbali hayawezi kufikiwa bila kuwa na takwimu za kuaminika.

Akizungumza alipotembelea banda la Ofisi ya Taifa ya Takwimu (Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) katika Maonesho ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba), Munde amesema Serikali inaendelea kuthamini mchango wa taasisi hiyo katika kukusanya, kuchambua na kusambaza takwimu zinazosaidia kufanya maamuzi sahihi ya maendeleo.

Amesema mipango yote ya maendeleo inategemea takwimu sahihi, akibainisha kuwa bila takwimu ni vigumu kupanga, kufuatilia na kutathmini utekelezaji wa miradi ya serikali.

“Mipango yetu haiwezi kwenda bila takwimu. Takwimu ndizo msingi wa kupanga, kufuatilia na kutathmini maendeleo ya taifa,” amesema Munde.

Aidha, ameipongeza NBS kwa kazi kubwa inayoifanya ya kuhakikisha nchi inapata takwimu sahihi, za wakati na zenye ubora, huku akiitaka taasisi hiyo kuendelea kudumisha weledi, uadilifu na uwazi katika kazi zake.

Kwa upande wao, viongozi wa NBS wamesema taasisi hiyo inaendelea kuimarisha mifumo ya ukusanyaji na uchakataji wa takwimu ili kusaidia Serikali katika kupanga sera, mipango na maamuzi yenye tija kwa wananchi.

Wameeleza kuwa takwimu sahihi zimekuwa chachu ya kuboresha huduma za kijamii na kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo nchini.

Ziara ya Naibu Waziri huyo katika banda la NBS ililenga kujionea shughuli mbalimbali zinazotekelezwa na taasisi hiyo pamoja na kupata maelezo kuhusu mchango wa takwimu katika ukuaji wa uchumi na ustawi wa jamii.