Waliokopa sh. bilioni 3.2 Mfuko wa Pembejeo wapewa siku 14 kuzirejesha
Na MWANDISHI WETU
Kampuni ya Udalali ya Yono Auction Mart, imetoa siku 14 kwa wananchi , taasisi na vikundi waliokopa pembejeo na fedha katika Mfuko wa Pembejeo (AGITF) kulipa madeni yao kabla ya kuchukuliwa hatua ikiwa ni pamoja na kufirisiwa mali zao.
Akizungumza na waandishi wa habari, Dar es Salaam, leo Mkurugenzi wa kampuni hiyo Dk. Scholastika Kevela, amesema amepewa maelekezo na serikali kupitia AGITF kuchukua hatua za kuuza mali za wadaiwa hao ambapo katika orodha hiyo kuna vigogo na wafanyabiashara wakubwa nchini.
Dk. Scholastika ameeleza, wadaiwa hao ni zaidi ya 200 ambao walikopa fedha na pembejeo mfuko huo wakiamini ni fedha za serikali zinatolewa bure hivyo kuto kurejesha.
“Serikali imeniagiza yoyote aliyechukua fedha katika Mfuko wa Pembejeo awe amerejesha ndani ya siku 14. Kama ulikopa uliwekeza nyumba tutauza fedha ya serikali irejeshwe,” amesema.
Amebainisha kiama hicho kitawakumba hata waliowadhamini wadaiwa hao kwani kwa mujibu wa sheria wanapaswa kulipa fedha hizo.
“Kwa niaba ya Mfuko wa Pembeje kama mdaiwa aliwekeza nyumba itauzwa ama kama aliwekeza gari kudhamini mkopo vitauzwa ili fedha ya serikali irejeshwe. Kukaa na fedha hii ni utovu wa fedha za umma,”amebainisha.
Aidha ameeleza operesheni ya kuzisaka na kuuza mali za wadaiwa hao itafanyika nchi nzima na katika orodha aliyokabidhiwa na serikali kuna vigogo, wafanyabiashara wakubwa na program kubwa za kilimo.
Reviewed by Gude Media
on
December 12, 2025
Rating:

.jpeg)