Dk. Mwigulu: viongozi wa dini endeleeni kutoa elimu ya umoja na amani
Atoa wito kwa Watanzania kuhimiza umoja na amani
Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchema ametoa wito kwa viongozi wa dini kuendelea kushirikiana na Serikali katika kutoa elimu ya umoja na amani, kupinga chuki, migawanyiko na vitendo vyovyote vinavyoweza kuvuruga mshikamano waTaifa.
Amesema kuwa vita yoyote inayohusisha wenyewe kwa wenyewe huwa haina mshindi bali ina kupoteza wote na mgawanyiko ndani ya taifa hauna mshindi bali una matokeo ya kushindwa wote kama Taifa.
Ametoa wito huo Alhamisi, Desemba 25, 2026) aliposhiriki ibada ya Sikukuu ya Krismasi iliyofanyika katika Kanisa Kuu la Kiinjili la Kilutheri la Azani Front jijini Dar es Salaam.
“Manufaa ya amani ni makubwa: huleta maendeleo ya kiuchumi, huimarisha ustawi wa jamii, na huwezesha kila Mtanzania kushiriki kikamilifu katika kujenga Taifa.”
Amesema kuwa Serikali inaendelea kutekeleza wajibu wake wakulinda amani na usalama wa nchi pamoja na kuwajenga Watanzania na hususani vijana kuthamini dhana ya uzalendo kwa nchi yetu.
“Tanzania imeendelea kuwa kielelezo cha umoja, amani, mshikamano na utulivu katika ukanda wetu na barani Afrika. Amani hii imejengwa juu ya misingi imara ya maadili, haki, kuheshimiana, uvumilivu na uzalendo.”
Kadhalika, Dkt. Mwigulu ametoa wito kwa wazazi na walezi kuendelea kushirikiana kwa karibu na taasisi za elimu na dini katika kuimarisha malezi ya watoto na vijana kwa kuwajengea misingi imara ya maadili na kuwaongoza kutumia vyema fursa za elimu, teknolojia na utandawazi kwa maendeleo yao na Taifa kwa ujumla.
Aidha, katika Ibada hiyo, Dkt. Nchemba ameungana na Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwatakia Wakristo na Watanzania wote kwa ujumla, Heri ya Sikukuu ya Krismasi na kuwasishi kusherehekea kwa Amani, Upendo na Utulivu, kudumisha mshikamano wa Kitaifa kwa maslahi ya Taifa la Tanzania.
Kwa upande wake, Mkuu wa Kanisa la Kiinjili na Kilutheri Tanzania (KKKT) na Mkuu wa Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Askofu Dkt. Alex Malasusa amekemea tabia za baadhi ya watu za kuchafua taswira za watu wengine, pamoja na kuichonganisha jamii. Kuna watu wakiona jamii imekaa pamoja kwa amani wao inawakosesha raha”.
Reviewed by Gude Media
on
December 25, 2025
Rating:

.jpg)

