Kinyerezi Day Kutoa Huduma za Kijamii kwa Siku Saba


Na MWANDISHI WETU

WAKAZI wa Kata ya Kinyerezi, Wilaya ya Ilala, wanatarajiwa kunufaika na huduma mbalimbali za kijamii zitakazotolewa kwa siku saba kupitia programu ya Kinyerezi Day, itakayozinduliwa Jumatatu, Oktoba 19, 2026.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Naibu Meya wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, John Mrema (WAHENGA), amesema programu hiyo imelenga kuwasogezea wananchi huduma muhimu karibu na maeneo yao ya makazi.

“Jumatatu, Oktoba 19, tunazindua Wiki ya Kinyerezi Day, ambayo itakuwa na siku saba za kutoa huduma mbalimbali kwa wananchi wa Kinyerezi ili kurahisisha upatikanaji wa huduma hizo karibu na makazi yao,” amesema Mrema.

Amesema huduma zitakazotolewa ni pamoja na kliniki ya usajili wa Vitambulisho vya Taifa (NIDA), elimu na huduma kuhusu mikopo ya asilimia 10, huduma za afya, kliniki ya ardhi, huduma za kisheria, bima ya afya pamoja na huduma za kibenki.

Mrema amewahimiza wakazi wa kata hiyo na wananchi wengine wa Wilaya ya Ilala, kujitokeza kwa wingi, kunufaika na huduma hizo.

Aidha, amesema shughuli hizo zitafikia kilele Jumamosi, Oktoba 24, 2026, wakati wa fainali za mashindano ya WAHENGA Super Cup. Fainali hizo zinatarajiwa kufungwa na Mkuu wa wilaya hiyo, Edward Mpogolo, ambaye anarajiwa kuwa mgeni rasmi.

Aidha finali za mashindano hayo zitafanyika katika Uwanja wa Kecha, uliopo karibu na Ofisi ya Mashtaka.