Na MWANDISHI WETU
WASHIRIKI wa Maonesho ya Wanasayansi Chikukizi Tanzania (YST) 2026, wamebuni miradi ya kisayansi inayolenga kutatua changamoto za jamii, zikiwemo mabadiliko ya tabianchi, afya, uhifadhi wa mazingira na matumizi endelevu ya rasilimali.
Akizungumza na waandishi wa habari, Dar es Salaam, Septemba 13, Mwanzilishi Mwenza wa YST, Dk. Gozibert Kamugisha amesema maonesho hayo yanatarajiwa kuwafinyika Septemba 17, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam katika Jengo Jipya la Maktaba, ambapo mgemi rasmi ni Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolfu Mkenda.
Dk. Kamugisha alisema miradi hiyo inatoa suluhisho kwa vitendo changamoto za maendeleo na baadhi yake ikihusu mifumo ya mifereji ya maji na ustahimilivu wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na mashine ya kuhifadhi nafaka kiotomatiki.
"Vijana nchini Tanzania wanaendelea kuonyesha uwezo mkubwa katika sayansi na ubunifu, huku miradi 1,330 ya kisayansi ikiwasilishwa mwaka huu kupitia programu ya Young Scientists Tanzania (YST), inayolenga kuwajengea wanafunzi wa shule za sekondari uwezo wa kutatua changamoto mbalimbali zinazoikabili jamii", amesema.
Dk. Kamugisha amesema miradi mingine inalenga uhifadhi wa mazingira, mfumo wa kudhibiti popo bila kuwaua, usafi wa maziwa yanayouzwa mijini na Dawa 'Track Biometric' kufuatilia utoaji wa dawa na watoa huduma za afya.
Amesema vijana hao wamewasilisha miradi inayolenga matumizi endelevu ya rasilimali za maji asilia, dawa za asili kwa ajili ya kuboresha afya ya binadamu, matumizi bora ya umeme na mbinu za kuongeza upatikanaji wa kaa wa baharini.
Pia amesema ongezeko la idadi ya maombi ya miradi ya sayansi mwaka huu, inaonyesha kuongezeka kwa hamasa miongoni mwa wanafunzi katika kujifunza, kufanya utafiti na kutumia sayansi kutafuta majibu ya changamoto za kijamii na kiuchumi.
"Katika kipindi cha miaka 16 iliyopita, jumla ya wanafunzi 22,568 na walimu 3,291 wamepata fursa ya kujifunza kuhusu sayansi na ubunifu kupitia programu ya YST ya kuwafikia wanafunzi shuleni", amesema.
Kwa upande wa Ofisa Mtendaji wa Karimjee Foundation, Caren Rowland, amesema taasisi hiyo imekuwa ikiunga mkono YST kwa miaka 16, katika kuchochea ari ya kujifunza sayansi, ubunifu na uvumbuzi miongoni mwa vijana wa Kitanzania.
Amesema kaulimbiu ya maonesho ya mwaka huu inalenga kuonesa namna sayansi na tekonolijia zinavyowatengenezea vijana fursa mbalimbali za kukuza uchumi na kuleta pamoja suluhisho la changamoto zilipo katika jamii zao.
Amesema kwa mwaka huu Karimjee Foundation itatoa ufadhili wa masomokwa vijana wengine wanne, watakaokuwa washindi wa jumla na kategoria ya mshindi wa elimu maalumu, hatua itakayoongeza nguvu katika dhamira yake ya kuwekeza kwa wanasayansi, wabunifu na viongozi wa Taanzania wa kesho.
Caren amesema maonesho ya YST yamekuwa jukwaa muhimu kwa vijana kuonesha vipaji, mawazo na uwezo wao wa kubuni na kutatua changamoto, huku sayansi na teknolojia zikitumika pia kufungua fursa za ujasiriamali, ajira na uwezeshaji wa kiuchumi.
Amesema Karimjee Foundation tayari imetoa ufadhili wa masomo kwa vijana 53 waliopata kushinda kupitia mashindano hayo, ambao wamewezeshwa kuendelea na elimu ya juu na kukuza zaidi maarifa na ujuzi wao.
"Karimjee Foundation haifadhili tu mashindano ya sayansi, tunawekeza katika kizazi kitakachobuni Tanzania ya kesho", amesema.
Caren amesema Karimjee Foundation inatambua na kuthamini juhudi, bidii, ubunifu na dhamira iliyooneshwa na washiriki wote wa YST. Kila kijana anayethubutu kuibua wazo, kufanya utafiti, kuandaa mradi na kuuwasilisha mbele ya wengine tayari anachangia katika kujenga utamaduni wa sayansi , ubunifu na uvumbuzi.