Na MWANDISHI WETU
Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, amewataka wananchi wanaoishi katika maeneo hatarishi, hususan mabondeni na kwenye mikondo ya maji, kuhama mara moja na kutafuta maeneo salama ili kuepusha maafa yanayoweza kusababishwa na mvua kubwa zinazotarajiwa kunyesha.
Mpogolo ametoa agizo hilo wakati wa ziara yake katika eneo la Viwege, ambapo alizungumza na wananchi wanaoishi katika mazingira hatarishi na kuwaeleza umuhimu wa kuchukua tahadhari mapema, hasa katika kipindi hiki ambacho mvua kubwa za El Nino zinatarajiwa kuanza.
“Mnafahamu kabisa kuwa maeneo haya mliopo hayaruhusiwi kuishi. Sasa ni vizuri katika kipindi hiki ambacho mvua hazijaanza mtafute mahali salama ili kuepusha maafa yanayoweza kutokea mvua zikianza,” alisema Mpogolo
Mpogolo aliambatana na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Elihuruma Mabelya na Katibu Tawala wa Wilaya ya Ilala, Charangwa Selemani, ambapo walitembelea maeneo ya Viwege na Mbondole, Kata ya Majohe, kwa lengo la kutathmini hali ya mazingira na kuchukua hatua za kuimarisha usalama wa wananchi.
Amesema katika kuhakikisha Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam linajiandaa kukabiliana na athari za mvua zinazotarajiwa,ambapo amemuelekeza Meneja wa Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA) Wilaya ya Ilala kuhakikisha mitaro na mabonde yanasafishwa ili kurahisisha upitishaji wa maji na kupunguza hatari ya mafuriko.
Aidha amesema Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania imeendelea kutoa tahadhari kuhusu uwezekano wa kuwepo kwa mvua za El Nino, huku wananchi wakihimizwa kuchukua tahadhari, ikiwemo kuhama katika maeneo ya mabondeni na maeneo mengine hatarishi.
Amesema wananchi wametakiwa kuzingatia maelekezo ya Serikali, kushirikiana na mamlaka husika na kuhakikisha wanachukua hatua mapema kwa ajili ya usalama wao, familia zao na mali zao.


