Waumini wa Kiislamu Waonywa Utapeli wa Hijja, Taasisi 19 Zathibitishwa Rasmi kupeleka Mahujaji


Na MWANDISHI WETU

Waumini wa dini ya kiislamu wametakiwa kuwa makini na taasisi zinazowahamasisha kuwapeleka katika ibada ya Hijja bila kuwa na uthibitisho kutoka ofisi hiyo.

Akizungumza katika Kongamano la Taasisi za Hijja Tanzaia (TAHAFE) na maonesho ya taasisi za Hijja, jijini Dar es Saalam, Katibu wa Mufti Sheikh Mussa Hemed, amesema angalizo hilo limalenga kuwakinga waumini dhidi ya taasisi zisizoaminika.

Hemed amesema taarifa za miaka iliyopita zimeonesha changamoto zilizojitokeza, pale waumini wanapozitumia taasisi zisizoaminika ambapo baadhi ya mahujaji walidai kupoteza fedha, baada ya kushindwa kusafiri kwenda kufanya ibada ya Hijja, licha ya kulipia gharama za safari.

“Ushauri kwa waumini kabla ya kukabidhi fedha kwa taasisi inayokusanya mahujaji, ni muhimu kuhakikisha taasisi hiyo imetambuliwa na mamlaka husika, ikiwemo mwamvuli wa TAHAFE, pia ina vibali vinavyotakiwa na ina historia nzuri ya kutoa huduma za Hijja,”amesema.

 Hemed amesema katika kipindi cha mwaka huu kupitia ofisi ya Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) imedhibitisha taasisi 19 ambazo zitatoa huduma za Hijja kwa mahujaji wanaotaka kufanya ibada hiyo.

“Ndugu waislamu ninaomba kuwaambia kuwa taasisi hizi ndizo zitakazohusika na utoaji wa huduma hii, hivyo tuwe makini na taasisi zingine ambazo zinajitangaza bila ya kuidhinishwa na mamlaka husika,”amesema.

 Katibu huyo amesema taasisi hizo ambazo haziaminiki zinaweza kutumia fursa ya maandalizi ya ibada hiyo ya Hijja kukusanya fedha kutoka kwa waumini bila kutoa huduma walizoahidi.

“Katika miaka ya nyuma Kulikuwa na taasisi ambazo zilikuwa zikijitangaza katika misikiti lakini shirikisho hili la TAHAFE limesaidia kuondoa utapeli huo,” amesema.

 Kwa upande wake Mwenyekiti wa (TAHAFE), Sheikh Abdallah Khalid, amesema tangu kuanzishwa kwa shirikisho hilo kumekuwepo na udhibiti mkubwa kwa waumini wa kislamu wanaotaka kwenda kufanya ibada ya Hijja.

“Zamani tulikuwa tunasikia tu mara mahujaji wameachwa uwanja wa ndege walikuwa wakienda kufanya ibada ya Hijja, lakini yote haya yalikuwa yanatokea kwa kuwepo kwa baadhi ya taasisi ambazo ni za kitapeli.Haya ni mafanikio makubwa yaliyopatikana tangu kuanzishwa kwa shirikisho hili, hivyo niwaombe waumini wa kislamu kuwa taasisi 19 ndizo ambazo zimepewa ruhusa ya kupeleka waumini wa kislamu kufanya Hijja na si taasisi zinginezo,” amesema.

 Kwa upande wake Mkurugenzi wa Idara ya Mashariki ya Kati katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Abdallah Kilima, amewataka waislamu kuondoa mtazamo wa kuwa kufanya ibada ya Hijja ni matajiri.

“Hii itabidi tuondoe mtazamo huu kwani Hijja si kwa watu maalumu kinachotakiwa ni kufanya makongamano ya aina hii ya kuwahamasisha waumini wa kislamu kwenda kufanya ibada hii 

“Kwetu sisi Tanzania tumepewa idadi ya watu 25,000 na Mamlaka ya Saudia Arabia kwenda kufanya ibada hii lakini kwa wanaokwenda hawazidi 5000 hivyo tunachotakiwa ni kuweka malengo ya kufanya ibada hii,”alisema.

 Balozi Kilima amesema kinachotakiwa ni kutoa elimu ya kuwaeleza waumini wa kislamu namna ya kujidunduliza fedha kidogo kidogo hadi kufanikisha ibada hiyo.