Na MWANDISHI WETU
HALMASHAURI ya Jiji la Dar es Salaam imeibuka kidedea katika Maonesho ya Wakulima ya Nanenane Kanda ya Mashariki yaliyofanyika Morogoro, baada ya kutwaa vikombe vya mshindi wa kwanza kwa Mkoa wa Dar es Salaam pamoja na mshindi wa jumla wa maonesho hayo kwa mwaka 2026.
Akizungumza wakati wa kufunga Maonesho ya Wakulima ya Nane Nane, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera na Uratibu, Watu Wenye Ulemavu, Profesa Palamagamba Kabudi, amesema lengo la Maonesho ya Nanenane ni kuwawezesha wakulima wadogo na wakubwa kiuchumi.
Profesa Kabudi alitumia fursa hiyo kuwapongeza wadau wote walioshiriki katika maonesho hayo, wakiwemo wenyeviti wa kamati zilizoandaa maonesho hayo, kwa mchango wao mkubwa katika kuhakikisha wananchi wengi wanavutiwa na kushiriki.
Aidha, aliwapongeza washiriki wote, wakiwemo waliopata ushindi na wale ambao hawakufanikiwa, akisema ushiriki wao ni sehemu muhimu ya kuendeleza sekta ya kilimo nchini.
“Serikali itaendelea kuhamasisha programu mbalimbali na mashamba darasa, kwani maendeleo ya kilimo yanahitaji ushirikishwaji wa sekta zote,” amesema Profesa Kabudi.
Aidha, amesema Serikali imeelekeza utekelezaji wa maagizo yaliyotolewa na Waziri Mkuu, Mwigulu Nchemba, wakati wa ufunguzi wa maonesho hayo, ikiwemo kuhakikisha Maonesho ya Nanenane Kanda ya Mashariki yanaendelea kuwa endelevu na washiriki wanaendelea kuwa wabunifu.
Pia, Profesa Kabudi ameagiza mikoa yote kuhakikisha teknolojia, mbinu na mambo mbalimbali yanayoonyeshwa katika maonesho hayo yanawafikia wananchi kupitia mashamba darasa.
Wakati huo huo, amewataka watu wanaojishughulisha na sekta binafsi kujiunga na mifuko ya hifadhi ya jamii ili waweze kunufaika na huduma mbalimbali, ikiwemo bima ya afya pamoja na mafao ya uzeeni.
Amesema Serikali inaendelea kuhamasisha Watanzania wote, hususan walio katika sekta binafsi, kujiunga na mifuko ya hifadhi ya jamii, ikiwemo Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), ili kujihakikishia usalama wa kijamii na mafao ya baadaye.
